Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ni muhimu ili watu watambue kuwa hakuna mlo kamili bila mbogamboga na matunda

Mwakaa wa 2021 umetengwa kwa ajili ya mbogamboga na matunda.Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo
© FAO-Magnum Photos/Alex Webb
Mwakaa wa 2021 umetengwa kwa ajili ya mbogamboga na matunda.Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo

Elimu ni muhimu ili watu watambue kuwa hakuna mlo kamili bila mbogamboga na matunda

Afya

Umoja wa Mataifa umeutangaza mwaka huu 2021 kuwa wa mbogamboga na matunda, lengo likiwa ni kuelimisha watu kuhusu umuhimu na faida za mbogamboga na matunda.  Zawadi Kikoti wa redio washirika Green FM ya wilayani Makete, mkoa wa Njombe Tanzania, anazungumza na baadhi ya wananchi kuhusu uelewa wao katika ulaji wa mbogamboga na matunda.

Mkoa wa Njombe, ni miongoni mwa mikoa iliyoko nyanda za juu kusini mwa Tanzania. Eneo hili linatajwa kuwa lenye rutuba ambalo lina mazingira mazuri ya kuweza kustawisha mbogamboga na matunda ya aina mbalimbali kama vile matufaa, parachichi na mengine mengi. Laicha ya hali hiyo, mkoa huu ni miongoni mwa maeneo yenye watu wenye utapiamlo, ukitajwa kuwa na asilimia 53.6 ya watu wake wenye utapiamlo.   

Subira Mbilinyi mkazi wa kijiji cha Tandala ni miongoni mwa watumiaji wa mbogamboga na matunda kutoka wilayani makete anasema changamoto kubwa waliyonayo wananchi ni kutojishughulisha na kilimo cha mboga mboga lakini pia kutotambua faida ya mboga mboga za matunda. 

“Mboga za majani pamoja na matunda ni faida kwangu. Ninavyojua ni wachache wanaojua faida za mbogamboga na matunda. Elimu ipite. Kwa sababu unakuta mtu anasema wacha nitumie tu hii mbogamboga kwa sababu mboga (kitoweo) nyingine sijapata. Lakini akijua umuhimu wa mbogamboga na matunda faida yake ni nini nadhani watatumia kwa wingi sana.” Anasema Subira. 

Naye Karista Peter mkazi wa kijiji cha Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe anasema, “mimi napendelea sana kisamvu kwa kuwa ni mboga ya asili. Inaleta nguvu mwilini na ni tamu. Ukiunga na karanga ni mboga tamu na ninaipenda. Inaendana na ugali au wali. Mimi napenda mboga za majani, ni kheri ukaninyima nyama ukanipa mboga ya majani.”