Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za dharura zichukuliwe kunusuru wakazi wa Tigray- Guterres

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanachua hatua kusaidia makumi ya maelfu ya wakimbizi waliokimbia eneo la Tigray nchini Ethiopia na kuingia Sudan.
© WFP/Leni Kinzli
Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanachua hatua kusaidia makumi ya maelfu ya wakimbizi waliokimbia eneo la Tigray nchini Ethiopia na kuingia Sudan.

Hatua za dharura zichukuliwe kunusuru wakazi wa Tigray- Guterres

Wahamiaji na Wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameendelea kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya hali inayoendelea kwenye eneo la Tigray nchini Ethiopia.

Taarifa ya msemaji wake iliyotolewa New York, Marekani Jumanne usiku imemnukuu akisema kuwa bado anazingatia umuhimu mkubwa wa ubia kati ya serikali ya Ethiopia na Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe wake uliomo nchini humo, ambao unashughulikia mahitaji ya kibinadamu ya wananchi wote walioathiriwa na mzozo  unaoendelea kwenye taifa hilo la pembe ya Afrika.

Bwana Guterres amesisitiza umuhimu wa kuendeleza hatua za dharura ili kupunguza janga la kibinadamu na kuchukua hatua zozote kulinda wale walio hatarini zaidi.

Amesema ni kwa mantiki hiyo anaunga mkono ushiriki chanya wa serikali ya Ethiopia wakati wa ziara ya majuzi nchini humo ya Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na viongozi wengine waandamizi wa Umoja wa Mataifa akiwemo msaidizi wa Katibu Mkuu katika masuala ya usalama Gilles Michaud na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, David Beasley. 

“Ushiriki huu kwenye mazungumzo umefanyika kwa mujibu wa wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuhakikisha kuna ufikiaji endelevu wa walio na mahitaji ya kibinadamu bila vikwazo vyovyote na bila upendeleo kwenye maeneo ya mzozo huko Tigray na katika kambi za wakimbizi wa ndani kwenye eneo hilo.,” amesema Guterres.

Kamishna Mkuu Grandi na wenzake walitembelea kambi ya wakimbizi ya Mai-Aini katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia, na kujionea hali ilivyo na akaiahidi serikali kusaidia kupunguza madhara ya hali hiyo kwa raia.