WFP yanusuru wanaokula rojo la ukwaju na udongo mweupe kutokana na njaa Madagascar

3 Februari 2021

Miaka mitatu mfululizo ya ukame kusini mwa Madagascar, imekuwa mwiba kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuwa mazao yamekauka na ongezeko la vimbunga vya mchanga kwenye ardhi yenye rutuba, limesababisha wakulima washindwe kupanda mazao na sasa wanakabiliwa siyo tu na njaa bali pia utapiamlo uliokithiri.

Taswira halisi ya njaa! Watoto wenye utapiamlo kwenye wilaya ya Amboasary, miongoni mwa watu 1,350,000 wanaokadiriwa kuwa na uhaba wa chakula katika wilaya 10 zinazokumbwa na ukame kusini mwa Madagascar. 

Ukame wa muda mrefu na uhaba wa maji katika maeneo mengi umesababisha watu kutembea mwendo mrefu kwenda kuteka maji ya baharini. 

Miongoni mwa waathirika ni Ikemba, anayeishi na watoto wake watano na wajukuu 7 katika kijiji kilicho ndani zaidi. “Bado tuna majani machache ya mdungusi kakati. Ninaposhindwa kwenda kuombaomba kwa jirani, nachimba majani ya mdungusi kakati bila uhakika wa kuyapata.Tunapokosa chochote, tunakunywa maji ya baharini. Ni mbayá kwa afya zetu, lakini hatuna jinsi kwa sababu tutasihnda njaa.” 

Hali ni mbayá katika kaya nyingine ambako wanaloweka ukwaju na kunywa rojo lake na udongo mweupe ,ingawa mlo huu hauna virutubisho vyovyote kwa miili yao. 

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, limechukua hatua ya kusambaza mgao wa chakula kwa kaya 787 ambapo Vola Marie ametembea kilometa 8  na mwanae kupokea msaada huo. 

Vola anasema wao ni mafukara na hawana chakula kwa sababu ya ukame na hawana chochote wanachoweza kufanya. 

Mkurugenzi wa WFP kanda ya Kusini mwa Afrika Lola Castro anasema, Idadi ya watu wasio na chakula na ya watoto wenye unyafuzi inaongezeka. Tunahitaji fedha na tunahitaji rasilimali ili WFP iweze kuongeza operesheni zake hadi maeneo ya kusini zaidi ya Madagascar.” 

Ingawa hivyo, mgao wa WFP umeleta nuru na sasa hata jikoni moto umewaka na wanufaika wameweza kupika mlo wenye lishe kwa familia zao.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter