Mwaka mmoja tangu COVID-19 iwe dharura ya umma, bado gonjwa hilo ni tishio

29 Januari 2021

Mwaka mmoja tangu ugonjwa wa Corona au COVID-19 utangazwe kuwa dharura ya afya ya umma duniani, bado gonjwa hilo limesalia kuwa hatari na kutishia siyo tu nchi maskini bali pia tajiri.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesu akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi hii leo amesema wakati anatoa tamko hilo  la dharura ya afya ya umma duniani ambalo ni onyo la ngazi ya juu zaidi chini ya sheria ya kimataifa, kulikuwa na wagonjwa wasiozidi 100 na hakukuweko na kifo chochote cha COVID-19 nje ya China.

“Wiki hii, tumefikia wagonjwa milioni 100. Wagonjwa wengi zaidi wameripotiwa wiki mbili zilizopita kuliko wiki 6 za mwanzo za janga hili. Mwaka mmoja uliopita nilisema kuna fursa ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi hivi, baadhi ya nchi ziliitikia wito na baadhi hazikuitikia,” amesema Dkt. Tedros.

 

Sasa kuna fursa nyingine

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema ingawa hivyo baadhi ya nchi hazikuitikia wito wake wa mwaka jana, sasa kuna fursa nyingine kupitia chanjo ya COVID-19 ambayo inaweza kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo. “Tusipoteze fursa hii.”

Novavax
Mtu ambaye amejitolea kwenye majaribio ya chanjo ya COVID-19 akipatiwa chanjo aina ya NOVAVAX

Janga la COVID-19 limefichua na pia kukandamiza zaidi ukosefu wa usawa duniani na sasa kuna hatari dhahiri kuwa mbinu zinazoweza kusaidia kumaliza janga la Corona, zinaweza kutumika kupanua zaidi pengo la ukosefu wa usawa.

Dkt. Tedros ametaja suala la uzawa kwenye chanjo ambalo linaweza kukidhi tu mahitaji ya muda mfupi ya kisiasa ambayo yatakuwa na madhara siku za baadaye akisema kuwa, “hatuwezi kumaliza janga hili pahala fulani bila kulimaliza kila pahala.”

Amekumbusha kuwa dunia imefikia wakati muhimu katika janga la Corona lakini vile vile katika historia ambapo kuna janga linalokumba pande zote, “je dunia inaweza kuwa kitu kimoja na kuchukua mwelekeo mmoja?”

Ametolea mfano kuwa pindi kijiji kinapokumbwa na moto, haina maana yoyote kwa kikundi kimoja cha watu kuhodhi vifaa vyote vya kuzimia moto kwa ajili ya nyumba zao. “Moto utazimwa haraka iwapo kila mtu akiwa na kifaa cha kuzima moto watashirikiana kwa pamoja. Chanjo nyingi zinaendelea kutengenezwa na kuthibitishwa kwa matumizi. Kutakuwepo na chanjo kwa kila mtu. Lakini kwa kuwa sasa chanjo bado ni chache, basi tunapaswa kuwa makini kuhakikisha siku 100 za awali za utoaji chanjo mwaka 2021 zinalenga wahudumu wa afya na wazee katika nchi zote.”

Ujumbe wa Dkt. Tedros kwa serikali

Dkt. Tedros ametoa wito kwa serikali kupatia chanjo wahudumu wa afya na wazee na chanjo za ziada zielekezwe kwenye kituo cha COVAX cha kuratibu usambazaji wa chanjo ili nchi nyingine nazo ziweze kupatia chanjo watu wao.

Ujumbe kwa wananchi

“Ujumbe kwa wananchi katika nchi ambazo zinaanza kutoa chanjo: Pazeni sauti zenu kuchechemua serikali zisambaze chanjo hizo. Iwapo hauko  hatarini sana kupata COVID-19, chonde chonde subiri wakati wako wa kupatiwa chanjo.”
 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Kenya kuhakikisha kuna mikakati endapo Virusi vya Corona vitazuka:WHO

Shirika la afya ulimwenguni WHO limeendelea kuzitaka nchi zote kuchukua tahadhari na kujiandaa dhidi ya virusi vya corona ambavyo tayari vimetangazwa kuwa dharura ya afya ya kimataifa vitazuka katika nchi zao.

Virusi vya Corona sasa vyatangazwa kuwa dharura ya kiafya ya kimataifa

Mkutano wa pili wa kamati ya dharura ulioitishwa hii leo mjini Geneva Uswisi na shirika la afya duniani, WHO, chini ya sheria za kimataifa za afya (IHR) (2015) kuhusiana na mlipuko wa virusi vya corona 2019-nCoV nchini China, umeutangaza mlipuko huowa virusi vya corona kuwa ni dharura ya kiafya ya kimataifa, PHEIC.