Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Michezo ya kompyuta yawezesha UN kupata maoni ya watoto kuhusu tabianchi

Kura bunifu ya maoni ya wananchi kuhusu tabianchi ilitumia mbinu bunifu na kushirikisha vijana walio na umri wa chini ya miaka 18.
UNDP Bhutan
Kura bunifu ya maoni ya wananchi kuhusu tabianchi ilitumia mbinu bunifu na kushirikisha vijana walio na umri wa chini ya miaka 18.

Michezo ya kompyuta yawezesha UN kupata maoni ya watoto kuhusu tabianchi

Tabianchi na mazingira

Hatimaye matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na Umoja wa Mataifa kwa wakazi wa dunia kuhusu udharura wa janga la tabianchi yametolewa hii leo huku asilimia 64 ya washiriki wakitambua umuhimu wa hatua za dharura dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuwepo kwa hatua mahsusi za makusudi ili kukabili janga la tabianchi linalokumba dunia hivi sasa.

Ukipatiwa jina la Kura ya maoni ya tabianchi, utafiti huo umekuwa ni mkubwa zaidi kuwahi kufanyika kusaka maoni ya watu, ukifikia takribani nusu ya wakazi wa dunia katika nchi 50, ambapo nusu ya washiriki wana umri wa chini ya miaka 18, kundi ambalo ni linaguswa zaidi na mabadiliko ya tabianchi lakini kwa kawaida halipigi kura katika chaguzi za kisiasa katika nchi zao.

Pata ripoti kamilifu hapa.

Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, ndio liliratibu kura hiyo ya maoni ambapo washiriki waliulizwa iwapo mabadiliko ya tabianchi ni suala la dharura duniani na iwapo wanaunga mkono sera 18 kuu za tabianchi katika maeneo sita ambayo ni: uchumi, nishati, usafirishaji, chakula na mashamba, maliasili na ulinzi wa watu.

Wanawake wakulima wilayani Kakonko nchini Tanzania waliopokea mafunzo kuhusu mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
UN News/Assumpta Massoi
Wanawake wakulima wilayani Kakonko nchini Tanzania waliopokea mafunzo kuhusu mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Matokeo ni vipi?

Matokeo ni kwamba watu wanataka sera pana zaidi kuliko sasa, mathalani katika nchi 8 zinazoongoza kwa utoaji wa hewa chafuzi kwenye sekta ya nishati, washiriki wengi wameunga mkono nishati rejelezi.

“Katika nchi 4 kati ya 5 zenye viwango vikubwa vya utoaji hewa chafuzi kutokana na matumizi ya ardhi na pia zina takwimu za kutosha, idadi kubwa waliunga mkono uhifadhi wa misitu na ardhi. Washiriki katika nchi 9 kati ya 10 zenye idadi kubwa ya wakazi mijini, waliunga mkono matumizi zaidi ya magari ya umeme, mabasi au baiskeli,” imesema ripoti ya matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa leo jijini New York, Marekani.

Mtawala Mkuu wa UNDP Achim Steiner akizungumzia matokeo hayo amesema ni dhahiri kuwa yameonesha uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa umma wa wananchi duniani kwenye hatua za dharura dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Vitalu vya miti ambayo inasaidia kukabiliana na mabadilliko ya tabianchi
FAO
Vitalu vya miti ambayo inasaidia kukabiliana na mabadilliko ya tabianchi

Amesema wanaounga mkono ni watu wa rika mbalimbali, utaifa mbalimbali, umri na hata kiwango tofauti cha elimu.

“Lakini zaidi ya yote, kura hiyo ya maoni inaonesha jinsi watu wanavyotaka watunga sera wao washughulikie janga hili. Kuanzia sera rafiki za kilimo kwa tabianchi, hadi kulinda maliasili na kuwekeza katika miradi isiyoharibu mazingira wakati huu wa kujikwamua kutoka janga la Corona au COVID-19. Kura hii ya maoni inaleta mbele sauti za watu katika mjadala kuhusu tabianchi,”  amesema Bwana Steiner.

Mkuu huyo wa UNDP ameongeza kuwa matokeo yanaashiria vile ambavyo nchi zinaweza kusonga kukabili changamoto za tabianchi kwa kutumia maoni ya wananchi.

Mbinu bunifu zilitumika kufikia wasiofikiwa kirahisi

UNDP inasema mbinu bunifu za utafiti zilitumika kuhakikisha dodoso linafikia hata wale ambao ni vigumu kufikiwa, mathalani kundi la walio na umri wa chini ya miaka 18.

Mbinu hizo ni pamoja na kusambaza kwenye dodoso katika mitandao ya michezo ya kompyuta inayopatikana kwenye simu za viganjani, mpango uliofanyika kwa kutumia wataalamu wa kura za maoni kutoka Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.

Maeneo yaliyoungwa mkono

Sera zimeungwa mkono kwa mapana zaidi, ambapo asilimia 54 wameunga mkono uhifadhi wa misitu. Asilimia 53 wameunga mkono nishati ya sola, upepo na nishati rejelezi.

Asilimia 52 wameunga mkono mbinu rafiki za kilimo zinazojali tabianchi ilhali asilimia 50 wametaka kuwekeza katika biashara na ajira ambazo haziharibu mazingira.

Profesa Stephen Fisher kutoka Idara ya Sosholojia katika Chuo Kikuu Oxford amesema, “utafiti huu, ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kufanyika ukihoji watu maoni yao kuhusu mabadiliko ya tabianchi, umetuonesha kuwa mitandao ya michezo ya kwenye simu au kiganjani, siyo tu inafikia watu wengi, bali pia inaweza kushirikisha watu wa makundi mbalimbali katika makundi tofauti kwenye nchi. Maoni ya Watu kuhusu Tabianchi yametupatia hazina ya kipekee ya takwimu kuhusu maoni ya watu ambayo katu hatujawahi kusikia.”

UNDP  inasema utafiti umedhihirisha uhusiano kati ya kiwango cha elimu cha mtu na matamanio yake kuhusu hatua kwa tabianchi.

“Kumekuwepo na utambuzi wa dharura ya tabianchi miongoni mwa watu waliopata elimu za Vyuo Vikuu kwenye nchi zote, kuanzia nchi za kipato cha chini kama vile Bhutan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hadi nchi tajiri kama vile Ufaransa na Japan,” limesema shirika hilo.