Yavunja moyo baada ya vimbunga  Idai na Chalane, Msumbiji sasa Eloise- UNICEF 

26 Januari 2021

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la kuhudumia watoto, UNICEF na mpango wa chakula duniani , WFP yamefika eneo la kati la Msumbiji ili kutoa msaada kwa manusura wa kimbunga Eloise kilichopiga Msumbiji mwishoni mwa juma wakati bado wananchi hawasahau madhila ya vimbunga Kenneth na Idai. 

Pascoa Almeida akiwa kwenye shule ya Samora Machel mjini Beira jimboni Sofala akisema amefika hapa baada ya nyumba yake kujaa maji kufuatia kimbunga Eloíse, kilichovuma kwa upepo wa kasi ya kilometa 160 kwa saa kwenye eneo hili na kusababisha vifo vya watu 6, huku watu 12 wamejeruhiwa ilhali watu Elfu 8 hawana makazi yao huku hektari 142,000 za mashamba ya mpunga zikiwa zimefurika. 

Mahitaji hapa kwa mujibu wa UNICEF ni makazi, chakula, matibabu na ulinzi ikizingatiwa kuwa watu 5,000 wamehamishiwa kwenye makazi ya muda kukwepa pepo kali na mvua kubwa. Kwenye eneo hili manusura  wanapatiwa mlo na malazi, 

Kwa sasa kimbunga Eloise kinaendelea kusonga maeneo ya ndani ya Msumbiji ambayo yalikumbwa na kimbunga Idai mwaka 2019 na kimbunga Chalane mwezi Desemba mwaka jana. 

Daniel Timme ambaye ni mtaalamu wa mawasiliano UNICEF nchini Msumbiji amefika Praia Nova, “Kama unavyoona, makazi ya muda yameharibiwa, usiku wa manane. Wananchi waliamua kuhamishia watoto na wazee shule ya jirani kwa kuwa maji ya baharí yalikuwa yanajaa na kuwasogelea. Paa la shule unayoona ndio kwanza lilikuwa limekarabatiwa baada ya kuharibiwa na kimbunga Idai.  

Na kwa jinsi alivyojionea, Timme anasema,  “Inavunja moyo kwa sababu kimbunga kimepiga tena kwa jamii zilizo hatarini ambazo zilipigwa na kimbunga kibaya zaidi Idai mwaka mmoja uliopita, hasa makazi ya mabanda hapa Beira. Na kisha kuna hatari ya mafuriko baada ya saa 72. Eneo hili ni bonde na liko karibu na bahari kwa hiyo ni hatari sana. Tumeshuhudia hili miaka miwili iliyopita na tunapaswa kufikiria kusaidia watu wa hap ana kusaidia kadri tuwezavyo mafuriko yatakapo fika na baada ya hapo ni hatari ya uwezekano wa mlipuko wa magonjwa kama vile kipindupindu. Kuna hali mbaya tena maeneo ya kati Msumbiji.” 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter