Skip to main content

UNICEF Zambia yatumia WASH kunusuru wakimbizi na wenyeji

Moja ya visima vitano vya maji vilivyojengwa katika wilaya ya Mazabuka nchini Zambia kama sehemu ya kusaidia shule, vituo vya afya kwenye maeneo yaliyokumbwa na ukame na pia kukabili ugonjwa wa COVID-19.
© UNICEF/UN0391492/Siakachoma/OutSet Media
Moja ya visima vitano vya maji vilivyojengwa katika wilaya ya Mazabuka nchini Zambia kama sehemu ya kusaidia shule, vituo vya afya kwenye maeneo yaliyokumbwa na ukame na pia kukabili ugonjwa wa COVID-19.

UNICEF Zambia yatumia WASH kunusuru wakimbizi na wenyeji

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Zambia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limechukua hatua kusaidia jimbo la Luapula lililoko mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kuwa na huduma za kujisafi na maji safi, WASH kwa lengo la kuondokana na magonjwa ya kuambukiza na pia kupatia watoto fursa ya kutosha ya kujifunza.

Katika kufahamu kile ambacho UNICEF imefanya, Mainza Kawanu, afisa mawasilano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Zambia, ametukaribisha kuungana naye katika safari kwenye miradi mbalimbali ya kuboresha huduma za maji safi na kujisafi, WASH, ambayo shirika hilo linatekeleza katika jimbo la Luapula mpakani mwa Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Mainza anasema miradi hiyo ni kwa ajili ya wenyeji na wakimbizi kwa kuzingatia jimbo hilo lipo mpakani mwa Zambia na DRC. Ni safari ya siku mbili kutoka mji mkuu wa Zambia Lusaka.

Kituo cha kwanza ni makazi ya wakimbizi ya Mantapala kwenye shule ya Mantapala B na mwenyeji wetu ni Glora Nyam Gyan, afisa wa UNICEF ambaye anasema, “shule ya Mantapala B ina wanafunzi 2886. Kabla ya kujenga mradi wa WASH, shule ilitumia bomba la maji na kituo cha afya na baadhi ya kaya kwenye makazi haya. Kwa upande wa vyoo, shule ili kuwa na mashimo 5 tu ya choo kwa watoto wote, ikimaanisha watoto 500 wa kike kwa choo kimoja na watoto 700 wa kiume kwa choo kimoja. Hii ina maana kama wewe ni mwanafunzi katika shule hii ya Mantapala na unataka kusaka maji na wakati huo huo unataka kutumia choo, basi muda mwingi wa masomo utapotea.”

UNICEF imeshajenga vyoo 15 na vingine 28 vipya vinaendelea kujengwa, ikimaanisha kwamba mradi wa WASH ukikamilika kutakuwepo na mazingira mazuri ya kusoma na hii ina maana kwamba watoto wanapokuja shule basi watakuwa wamekuja kufanya kile wanachopaswa kufanya, yaani kujifunza.

UNICEF imebisha hodi pia kwenye kaya ambapo Gloria anasema kuwa shirika hilo linasaidia ujenzi wa zaidi ya vyoo elfu 2 kwenye makazi ya Matampala, “ili jamii ya hapa iweze kujifunza tabia za usafi na kujisafi ambazo ni muhimu kwa ajili ya usafi na kujikinga na magonjwa yanayoenezwa na ukosefu wa maji na hivyo waweze kuwa wazalishaji wenye tija.”

Sasa Mainza anasema tumeingia kijiji cha Kamwangila katika wilaya ya Chilenge jimboni Luapula, kijiji ambacho ni maarufu kwa kilimo cha mihogo na uvuvi.

Kisima cha kwanza kabisa cha maji kujengwa katika kijiji cha Chikwala wilaya ya Mazabuka jimboni Luapula nchini Zambia. Ni chanzo cha maji safi na salama kwa kaya 600.
© UNICEF/UN0391492/Siakachoma/OutSet Media
Kisima cha kwanza kabisa cha maji kujengwa katika kijiji cha Chikwala wilaya ya Mazabuka jimboni Luapula nchini Zambia. Ni chanzo cha maji safi na salama kwa kaya 600.

Katika kijiji hiki UNICEF imejenga kisima cha maji kinachohudumia familia zaidi ya 50 ambapo Margaret Chisenga ni mkazi wa eneo hili ambaye anasema “tulikuwa na matatizo mengi sana hapa kwa sababu ya ukosefu wa maji. Tulikuwa tunatembea umbali mrefu kutafuta maji. Na hata ukifika kisimani watu walikuwa ni wengi mno. Tunashukuru sana UNICEF kwa kutusogezea maji hapa karibu. 

Kutoka Kamwangila, Mainza anatusogeza hadi kijiji cha Nsamiwa chenye wakazi 720,  lakini jimboni humu humu Luapula, ambako UNICEF imetekeleza ahadi yake kwa kaya 102 za kijiji hiki kama anavyoelezea Noala Skinner, mwakilishi mkazi wa UNICEF Zambia.

Bi. Skinner anasema “tulitembelea hapa na ugeni kutoka Ujerumani mwaka 2019 na tuligundua kuwa walishaanza kutekeleza mradi wa kijiji wa   kujisafi lakini walikuwa wanatumia kisima cha wazi cha kizamani. Tuligundua kuwa kinafanya kazi na kina maji safi lakini si salama. Tuliahidi uongozi kuwa tutarejea pindi tutakapokuwa tumekamilisha kisima kipya na leo tumefika hapa na pale ndipo kuna kisima kipya.”

Kisima hicho ni salama na pamoja na uchimbaji wa visima, UNICEF imegawa miche 390,000 ya sabuni kwa wenyeji na wakimbizi kama sehemu ya mkakati dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19, sambamba na kuweka vituo vya kunawa mikono kwa maji na sabuni kwenye makazi ya kupokea wakimbizi.