COVID-19 ni somo kwamba, hatuwezi kumudu kupuuza hatari tunazozifahamu :Guterres 

25 Januari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la Corona au COVID-19 ni somo tosha la kukumbusha kwamba dunia haiwezi kumudu kupuuza hatari inazozijua. 
 

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa kimataifa wa mnepo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi ulioandaliwa nchini Uholanzi na kufanyika mtandaoni kuanzia leo Januari 25 hadi kesho Januari 26, Bwana. Guterres amesema mwaka huu umeanza kwa kumbusho la umuhimu wa kuwa na mnepo wa kukabili changamoto zinazoikabili dunia. 

Amesema “changamoto ya tabianchi ni hatari ambayo sote tunaitambua. Sayansi imeweka bayana kwamba tunakabiliwa na dharura ya mabadiliko ya tabianchi. Tayari tunashuhudia matukio yasiyo ya kawaida ya mabadiliko ya hewa ambayo yanaathiri Maisha na uwezo wa watu kuishi katika barara yote.” 

Ameongeza kuwa hali hii haiwezi kupuuzwa tena kwani kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO, kumekuwa na majanga zaidi ya 11,000 ambayo yametokana na hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi na maji katika miaka 50 iliyopita na kuigharimu dunia takribani dola trilioni 3.6. 
Majanga hayo pia yamekatili maisha ya wazi zaidi ya 410,000 katika muongo mmoja uliopita wengi wao wakiwa ni kutoka katika nchi za kipato cha chini na cha kati. 

Mafuriko nchini Uganda ambako nyumba zimezama.
UN News/ John Kibego
Mafuriko nchini Uganda ambako nyumba zimezama.

Kuhimili na kuwa na mnepo ni lazima 

Guterres ameongeza kuwa “ndio sababu nimetoa wito wa kuhakikisha tunahili na kuwa na mnepo dhidi ya janga hili. Tunahitaji matrilioni yadola za walipa kodi kufadhili juhudi za kujikwamua na janga la COVID-19 ili kuanza kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kujenga mustakabali wenye mnepo tunaouhitaji.” 
Hata hivyo amesisitiza kwamba kujikwamua huko kusiwe ni kwa nchi zilizoendelea pekee. 
“Lazima tupanue wigo wa ukwasi na mikakati ya kupunguza madeni kwa nchi zinazoendfelea na za kipato cha kati ambazo hazina rasilimali za kufufua uchumi wao kwa njia endelevu na jumuishi,”  amesema Katibu Mkuu.

Vipaumbele vitano vya kuzingatia 

Katibu Mkuu amesema anaona kuna mambo matano ya kuyapa kipaumbele kwa ajili ya kuhimili na kujenga mnepo. Mosi, nchi wahisani na benki za maendeleo za kitaifa, kikanda na kimataifa zinahitaji kuongeza kiasi na utabiri wa fedha zao kwa ajili ya kujenga mnepo, uhimili na uthabiti. 

Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu pengo la mabadiliko ya tabianchi inahesabu gharama za kila mwaka katika nchi zinazoendelea [pekee kuwa katika kiwango cha dola bilioni 70. Na kiwango hicho kinaweza kufikia kati ya dola bilioni 140 hadi bilioni 300 ifikapo mwaka 2030 na dola bilioni 280 hadi dola bilioni 500 mnamo mwaka 2050. 
Lakini bado kunasalia na pengo kubwa la ufadhili katika suala la kuhimili kwenye nchi zinazoendelea. “Ndio maana nimetoa wito wa asilimia 50 ya jumla ya sehemu ya ufadhili wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinazotolewa na wahisani wote na benki za maendeleo za nchi nyingi zigawanywe kwa ajili ya kuhimili na kujenga mnepo. Uhimili hauwezi kuwa nusu iliyopuuzwa ya mabadiliko ya tabianchi." 

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP linasema hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inaendelea kuzorota kwa kazi wakati mwimbi la njaa likienea katika nchi ambayo ina mgogoro, mvua kubwa na mafuriko.
Image captured from a WFP video
Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP linasema hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inaendelea kuzorota kwa kazi wakati mwimbi la njaa likienea katika nchi ambayo ina mgogoro, mvua kubwa na mafuriko.

Ameongeza kuwa Benki ya maendeleo Afrika ikiweka mfano mwaka 2019 kwa kutenga zaidi ya nusu ya fedha zake za ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kujenga uhimili na mnepo.Hivyo “Nawahimiza wafadhili wote na Benki za maendeleo za kimataifa kujitolea kwa ajili ya lengo hili na COP26 na kulifikia ifikapo mwaka 2024. Nakaribisha kujitolea kwa leo kwa serikali ya Uholanzi. Na hebu tukumbuke kwamba nchi zilizoendelea ni lazima zifikie ahadi ilizozitoa kwenye makubaliano ya Paris za kukusanya dola bilioni 100 kwa mwaka kwa ajili ya kukabiliana na kujenga uhimili na mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea.” Pili, bajeti zote zitakazotengwa na maamuzi ya uwekezaji yanahitaji kuzingatia mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 

Hatari ya mabadiliko ya tabianachi lazima iingizwe katika michakato yote ya ununuzi haswa kwa miundombinu. 
Nchi zinazoendelea lazima zipate msaada na nyenzo muhimu ili kufikia lengo hili. Mfumo wa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi hizi. Tatu, tunahitaji kuongeza kwa kiasi kikubwa nyenzo za uwezeshaji wa kifedha kwa ajili ya athari ziliazosababishwa na majanga kama vile kituo cha bima ya hatari za majanga Caribbea na kitengo cha Afrika cha ujenga uwezo wa kuhimili hatari za majanga. 

Guterres amesema “Natoa wito pia kwa wafadhili , Benki za maendeleo kila konda na taasisi za fedha za binafsi kufanya kazi nan chi zilizo katika mazingira magumu katika kuunda vyombo vipya vya kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa uhimili na mnepo. Kwani kwa kila dola inayowekezwa katika miuondombinu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi , dola sita zinaweza kuokolewa.” Nne, tunahitaji kupunguza changamoto za fursa za upatikanaji wa fedha hasa kwa walio hatarini zaidi na kupanua wigo wa mipango ya kupunguza madeni. 

Katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea za visiwa vidogo jumla ya fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi bado ni ndogo zikiwakilisha asilimia 14 tu asilimia 2 tu ya upatikanaji wa fedha hizo mtawaliwa. 
Nchi hizi ziko mstari wa mbele wa mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, lakini kwa sababu ya ukubwa na vikwazo vya uwezo walio nao zinakabiliwa na changamoto kubwa za kupata fedha za kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 

Hivyo Katibu Mkuu amesisitiza “Ni lazima kuwe na juhudi za pamoja kuweza kuondoa vizuizi hivi.” Tano, na mwisho  tunahitaji kuunga mkono mikakati ya kikanda ya juhudi za kuhimili na kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 

Hii itaruhusu kwa mfano kubadilishana madeni mfano kwa visiwa vya Karibbea au visiwa vya Pasifiki, na kutoa ukwasi unaohitajika kwa nchi zilizo katika mazingira magumu ambazo zinahitaji saana msaada. 

Bwana Guterres amesisitiza kuwa msaada wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujenga ,mnepo ni sharti la kimaadili, kiuchumi na kijamii. Leo hii mtu mmoja kati ya watatu bado hajafanikiwa vya kutosha kufikiwa na mifumo ya kutoa tahadhari ya mapema na njia za kufikisha taarifa katika kiwango kinachohitajika. 

Kwa mantiki hiyo “Tunahitaji kufanyakazi kwa pamoja kuhakikisha ufikishaji wa taarifa na tahadhari ya mapema unamfiukia kila mtu ili kusaidia kupunguza athari za majanga ya mabadiliko ya tabianchi na hasara zake. Tuna nyenzo, tuna ujuzi na tuna fursa za kutimiza haya kwa haraka zaidi na vyema zaidi ili kujenda uhimili na mnepo . Natumai mkutano huu utasaidia kufikia muafaka unaohitajika katika kuhakikisha uhimili na kujenga mnepo  na pia kutuelekeza kwenye matokeo mazuri tunayoyatamani kwenye mkutano wa COP26.” 
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter