Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukivuruga elimu, umemvuruga kila kitu na kila mtu:UN

Mwalimu na wanafunzi wake wakifanya majaribio ya kufungua shule wakati wa COVID-19 kwa kuzingatia masharti kama uvaaji barakoa na umbali kati ya mtu na mtu kwenye shule ya msingi Phom Penh Cambodia
© UNICEF/Seng
Mwalimu na wanafunzi wake wakifanya majaribio ya kufungua shule wakati wa COVID-19 kwa kuzingatia masharti kama uvaaji barakoa na umbali kati ya mtu na mtu kwenye shule ya msingi Phom Penh Cambodia

Ukivuruga elimu, umemvuruga kila kitu na kila mtu:UN

Utamaduni na Elimu

Katika siku ya kimataifa ya elimu hii leo Umoja wa Mataifa umesema endapo elimu inaingiliwa na kuvurugwa basi inamuathiri kila mtu hususan wanafunzi, waalimu na familia.

Kupitia ujumbe wake maalum kwa siku hii ya elimu ambayo kila mwaka huadhimishwa Januari 24, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema“Nawashukuru sana kwa ujasiri wao wakati wa janga hili la coronavirus">COVID-19 ambalo katika kilele chake lililazimisha karibu kila shule, taasisi na vyuo vikuu kufunga milangoyake.”

Ameongeza kuwa ingawa usumbufu huu umesababisha ubunifu katika njia za kujifunza na kusoma, pia umepunguza na kukatisha matumaini ya mustakbali bora miongoni mwa watu walio katika jamii za mazingira magumu.

Watoto katika shule nchini Haiti wakipata chakula kama sehemu ya mpango wa mlo shuleni wa WFP.
UN Photo/Leonora Baumann
Watoto katika shule nchini Haiti wakipata chakula kama sehemu ya mpango wa mlo shuleni wa WFP.

Sote tunalipa gharama

Guterres amesema bila shaka elimu ni msingi wa kupanua wigo wa fursa, kubadili uchumi, kupambana na hali ya kutivumiliana, kulinda sayari yet una kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Kwa mantiki hiyo ameongeza kuwa“Wakati dunia ikiendelea kukabiliana na janga hili la COVID-19, elimu kama haki ya msingi na faida ya umma wa kimataifa ni lazima ilindwe ili kuepuka zahma kubwa kwa kizazi hiki.”

Amesisitiza kwamba hata kabla ya janga la COVID-19 watoto na vijana barubaru milioni 258 hawakuwa wakihudhuria shule na asilimia kubwa ni wasichana.

Kwa mujibu wa takwimu zaidi ya nusu ya watoto wa umri wa miaka 10 katika nchi za kipato cha chini cha wastani hawakuweza kujifunza kusoma vitu vya kawaida kabisa.

Mwaka 2021 Guterres amesisitiza “Ni lazima tutumie furs azote kubadili hali hii. Ni lazima tuhakikishe tunatunisha tena mfuko wa ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya elimu na kuimarisha ushirikiano wa kimatifa kwa ajili ya elimu.”

Pia amesema ni lazima“Kuimarisha juhudi zetu za kufufua elimu, tutoe mafunzo kwa waalimu, kuziba pengo la kidijitali na kutafakari upya mitaala ya elimu ili kuwawezesha wasomaji kwa ujuzi na elimu itakayowawezesha kushamiri katika dunia hii inayobadilika kwa kasi. Hivyo hebu tuahidi kuchagiza elimu kwa wote leo na kila siku.”