Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO ni familia ya mataifa, na tuna furaha Marekani inasalia kwenye familia-WHO

Dkt. Anthony Fauci mwanasayansi wa Marekani (kwenye skrini) na Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO wakati wa kikao cha bodi ya WHO.
WHO
Dkt. Anthony Fauci mwanasayansi wa Marekani (kwenye skrini) na Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO wakati wa kikao cha bodi ya WHO.

WHO ni familia ya mataifa, na tuna furaha Marekani inasalia kwenye familia-WHO

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani ,WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amekaribisha hatua ya Rais wa Marekani Joe Biden ya kuirejesha tena Marekani kushirikiana na shirika hilo.

Akizungumza kwenye mkutano wa wanabodi wa shirika hilo, Dkt. Tedros amekaribisha Dkt. Anthony Fauci anayeongoza ujumbe wa Marekani kwenye kikao hicho cha 148 na kumshukuru kwa msaada wake kwa miaka mingi na hususan mwaka uliopita. Aidha amempongeza kwa uongonzi wake wakati wa kukabilian na janga la COVID-19 Marekani. 

Dkt. Tedros amesema, “leo ni siku njema kwa WHO, na siku njema kwa ajili ya afya ya dunia. Ninatuma shukrani za dhati na pongezi kwa rais Biden na naibu wake Harris na kwa wamarekani. Asante rais Biden kwa kutimiza ahadi ya kusalia kwa marekani kama mwanachama wa WHO.” 

Mkurugenzi Mkuu huyo pia ameshukuru Marekani kwa dhamira yake ya kutumia vifaa vya kukabiliana na COVID-19 na COVAX na kurejelea umuhimu wa kufanya kazi pamoja kama familia moja kuhakikisha kwamba nchi zote zinaanza kutoa chanjo kwa wahudumu wa afya wake na makundi mengine yaliyo hatarini katika siku 100 za kwanza za mwaka huu wa 2021. 

Tangu kuanzishwa kwa WHO mwaka 1948, Marekani imekuwa na mchango muhimu katika afya ya kimataifa na watu wamarekani wamekuwa na  mchango mkubwa kwa afya ya watu ulimwenguni.  

Dkt. Tedros amesema kuna kazi nyingi ya kufanya na megni ya kujifunza ili kutokomeza janga hili na kukabiliana na changamoto nyingi za afya zinazotukabili, lakini dunia itaweza kuzikabili kwa ushirikiano wenu. 

Halikadhalika Dkt. Tedros ameelezea utayari wa WHO kusaidia Marekani kwa msaada wa sayanzi, suluhu na umoja na huduma na kwamba, “WHO ni familia ya mataifa, na tunafuraha kwamba Marekani inasalia kwenye familia.”