Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa ombi la dola milioni 76 kwa ajili ya mahitaji ya dharura Madagascar

Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.
WFP/Tsiory Andriantsoarana
Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.

UN yatoa ombi la dola milioni 76 kwa ajili ya mahitaji ya dharura Madagascar

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa nchini Madagascar umetoa ombi la dharura la dola milioni 76 kwa ajili ya kusaidia takriban watu milioni moja ambao wanakabiliwa na janga la kibinadamu na wanahitaji chakula, lishe, maji na vifaa vya kujisafi na huduma ya afya. 

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Matiafa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA eneo la Grand Sud ambalo limelengwa katika ombi hilo, msimu wa kilimo umeharibiwa kutokana na ukame mbay zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka kumi ikiwa ni ukame kwa mara ya tatu mfululizo. 

Uwepo wa Janga la COVID-19 na athari kutokana na vikwazo vimeathiri maeneo mengi ya nchi, na hivyo kupelekea watu katika hali mbaya. 

Mtu mmoja kati ya watatu maeneo ya kusini hana yhakika wa chakula huku mbinu za kuishi wakati wa ukame ambazo zinajumuisha wanafamilia kwenda mjini kupata ajira zimegonga mwamba kutokana na vikwazo wakati wa janga ambazo zilikwamisha usafiri kutoka eneo moja hadi lingine. 

Hali ya ukosefu wa uhakika wa chakula kutoka mwezi uliopita inaonesha kwamba zaidi ya watoto 135,000 walio chini ya umri wa miaka 5 wanakadiriwa kuwa na utapiamlo uliokithiri katika kipindi cha miezi michahce ijayo katika eneo la Grand Sud. 

Ombi hilo la dharura linajazia hatua za kitaifa na linalenga mahitaji ya dharura ya jamii katika eneo la Grand Sud katika msimu wa kiangazi. Iwapo ufadhili utapatikana utasaidia kuimarisha uhakika wa chakula kwa watu milioni 1.1, kuhakikisha maji kwa watu 420,000 walio hatarini, kutoa msaada wa lishe kwa watoto 300,000 walio chini ya umri wa miaka 5 na kuhakikisha huduma ya afya kwa watu 230,000.