Chanjo ya COVID-19 yaanza kutolewa kwa wakimbizi nchini Jordan 

Watoto wakimbizi katika kambi za Zaatari nchini Jordan wakionyesha ishara ya amani
UN Photo/Sahem Rababah
Watoto wakimbizi katika kambi za Zaatari nchini Jordan wakionyesha ishara ya amani

Chanjo ya COVID-19 yaanza kutolewa kwa wakimbizi nchini Jordan 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakimbizi nchini Jordan wameanza kupokea chanjo ya COVID-19 ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa afya ambao unajumuisha raia wote, wakimbizi na wakazi.

Wakimbizi 43 kutoka kambi ya Wakimbizi ya Al-Zaatari wamepokea chanjo katika katika kituo cha magonjwa kilichoko Mafraq, mji ulio karibu na kambi hiyo. Mipango ya wengine zaidi kuchanjwa inaendelea. 

Shirika la la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limekuwa likisaidia juhudi za serikali ya Jordan ambayo kupitia Wizara yake ya afya wamezindua kampeni ya chanjo katika vituo 29 vya afya kote nchini.  

UNHCR imekuwa ikisaidia katika kuhamasisha na kusaidia wakimbizi kujiandikisha kwa ajili ya kupokea chanjo na pia kwa kuwapatia usafiri wa kufika kwenye kiliniki za afya pale inapohitaji.  

Zaidi ya watu 200,000 (laki mbili) wamesajiliwa katika mfumo wa serikali na UNHCR hivi sasa inafahamu kuwa wakimbizi 53 wameshapewa miadi ya kuchanjwa  

Kama sehemu ya mpango wa kitaifa wa chanjo ya COVID-19 ya nchi hiyo, mtu yeyote anayeishi kwenye ardhi ya Jordan, pamoja na wakimbizi na wanaotafuta hifadhi, anastahili kupokea chanjo hiyo bila malipo. Wakimbizi ambao wako katika moja ya makundi maalumu  ya vipaumbele kitaifa,  watapokea chanjo mwanzoni. Wengine wanaweza kufuata kwa kadri utoaji chanjo utakavyoongezwa. 

UNHCR inasema inaendelea na kampeni katika ngazi za nchi, kikanda na ulimwengu kwa ajili ya wakimbizi na watu wengine inaowalinda kujumuishwa katika mikakati ya kitaifa. Kuhakikisha, kama kipaumbele, chanjo zinapatikana kwa walio hatarini zaidi, kama wazee, wale walio na magonjwa sugu, au watu ambao wana kinga ndogo, pamoja na wafanyakazi wa sekta ya afya na wengine walio na kazi muhimu za kimfumo. 

Fatima Abdulkarim Al-Aloul raia wa Syria, ni mmoja wa wakimbizi wazee nchini Jordan waliofanikiwa kupata chanjo ya COVID-19, na kimsingi ndiye anakuwa mkimbizi wa kwanza kutoka kambi ya Al-Zaatari  anasema, “ninatoa wito kwa kila mtu kupokea chanjo. Kwa mapenzi ya Mungu, kwa afya njema na usalama.”  

Jordan ambayo ni mwenyeji wa wakimbizi wapatao 750,000 waliosajiliwa na UNHCR, ilianzisha hatua kali zaidi wakati wa kipindi cha mwanzo cha janga la virusi vya corona katika jaribio la kuzuia kuenea kwa virusi. 

Idadi ya wakimbizi ambao walikutwa na virusi vya COVID-19 nchini Jordan imebaki chini kwa asilimia 1.6, ikilinganishwa na asilimia tatu miongoni mwa watu wa Jordan. 

UNHCR inasema, tangu kuanza kwa janga la COVID-19, wakimbizi wamejumuishwa kiukarimu katika Serikali ya Jordan mpango wa kitaifa wa serikali ya Jordan wa kukabiliana na ugonjwa na hivyo wakimbizi kw ana uwezo wa kupata huduma ya afya na matibabu sawa kabisa na raia wa Jordan.