Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila amani hakuna haki na bila haki hakuna amani, King tutakuenzi daima:UN 

Hayati Dkt. Martin Luther King Jr. akizungumza na wanahabari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani mwaka 1967.
UN /Teddy Chen
Hayati Dkt. Martin Luther King Jr. akizungumza na wanahabari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani mwaka 1967.

Bila amani hakuna haki na bila haki hakuna amani, King tutakuenzi daima:UN 

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umesema mchango na mtazamo wa Martin Luther King Jr aliyekuwa mwanaharakati mkubwa wa haki za binadamu duniani kutakumbukwa na kuenziwa daiama hasa katika zama hizi ambazo dunia imegawika mapende, ukiukwahi wa haki za binadamu unaendelea na chuki na ubaguzi vikimea mizizi. 

Kupitia ujumbe maalum wa njia ya video kwenye kituo cha King leo Januari 18 ikiadhimishwa siku ya kuzaliwa ya nguli huyo wa kupigania haki za binadamu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amekumbusha kwamba mwaka 2020 ulikuwa ni mwaka wa zahma kwani maisha ya mamilioni ya watu kote duniani yamepotea, shughuli zimesismama kutokana na janga la corona au COVID-19 na athari za janga hilo hazisemeki. 

Ameongeza kuwa “Maisha ya watu yamesambaratika, huku maadili ya pamoja yakiwekwa kwenye mtihani mkubwa na kjanga hilo kudhihirisha mizizi ya pengo la usawa katika jamii zetu. Watu kutoka jamii za wachache ndio walioathirika zaidi kama ilivyo kwa wengine walio wachache katika jamii zetu. Lakini pia kusambaa kwa virusi hivyo vya corona kumetoa mwanya mpya kwa mitandao ya kijamii kusambaza chuki na taarifa za uongo na hata kabla ya janga hilo dunia ilikuwa inakabiliwa na wimbi la kauli za chuki, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, unazi wa kisasa, fikra za kuwa wazungu ni bora kuliko wengine na mifumo mingine ya ubaguzi .” 

Sasa ni wakati wa mshikamano 

Bi. Muhammed amesisitiza kuwa sasa ni wakati wa umoja, mshikamano na utu na maadili ya Umoja wa Mataifa ndiyo yatakayoongoza njia. 

Ameongeza kuwa kama Dkt. King alivyoukumbusha ulimwengu katika hotuba yake ya kihistoria mbele ya Umoja wa Mataifa mwaka 1967 kwamba “Hakuwezi kuwa na haki bila amani na hakuwezi kuwa na amani bila haki. Na ukweli huo bado una mashiko makubwa hadi leo hii .” 

 Na kwa mantiki hiyo amesisitiza kwamba wakati dunia ikihaha kujikwamua na kujijenga upya kutoka kwenye janga hili la COVID-19 na kujenga dunia bora zaidi “Tunahitaji kuwa na tofauti mpya ambayo ni jumuishi na endelevu. Hii inamaanisha kwamba kuwekeza katika mahusiano ya kiujamii na kusongesha mbele ufikiaji wa usawa na fursa kwa wote.” 

  Amesema urithi wa mtazamo wa Dkt. Martin Luther King na viongozi wengine Wamarekani weusi ambao ni wa kutetea haki za binadamu kama vile mbunge wa congress John Lewis kutoka Atlanda ambaye alijitolea kupigania usawa wa rangi au Ralph Bunche a,mbaye alipokea tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1950 kutokana na kazi yake kama mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Palestina , na mchango wake utaendelea kutuhamasisha katika safari hiyo . 

 Dkt. King alikumbatioa maudhui ya UN 

Naibu Katibu Mkuu amesema Dkt. King aliishi kwa kukumbatia maadili ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amani, haki ya kijamii na haki za binadamu. 

Hivyo ameitaka dunia ikitumia maadhimisho haya ya siku ya King kusisitiza ahadi ya kazi aliyokuwa akiifanya “Hebu na kupate nguvu kutoka kwa maneno ya Dkt. King yasemayo Giza haliweli kufukuza giza, ni mwangaza pekee ndio unaoweza kufanya hivyo. Chuki haiwezi kufukuza chuki ni upendo pekee ndio unaoweza kufanya hivyo.” 

Ameahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa mdau mkubwa wa kuendeleza matakwa na kazi ya Dkt. Martin Luther King Jr.