Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani mwingine wa UN auawa CAR, wawili wajeruhiwa

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini CAR wakiwa doria kwenye jimbo la Mbomou
MINUSCA/Leonel Grothe
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini CAR wakiwa doria kwenye jimbo la Mbomou

Mlinda amani mwingine wa UN auawa CAR, wawili wajeruhiwa

Amani na Usalama

Mlinda amani mwingine wa Umoja wa Mataifa kutoka Burundi ameuawa leo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na wengine wawili wamejeruhiwa, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametoa taarifa jijini New York, Marekani hii leo ikisema kuwa shambulio hilo linadaiwa kufanywa na kikundi kiitwacho Coalition des Patriotes pour le Changement (CPC) ambao walishambulia msafara wa walinda amani wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA kwenye eneo la Grimari jimboni Ouaka.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mlinda amnai huyo na wananchi na serikali ya Burundi huku akiwataki ahueni ya haraka walinda amani waliojeruhiwa.

Bwana Guterres amerejelea kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita huku akitoa wito kwa mamlaka nchini CAR kutumia uwezo wake wote kusaka wahusika wa shambulio hilo ili wafikishwe mbele ya sheria.

Katibu Mkuu amesema mashambulizi dhidi ya walinda amani hayapaswi kukwepa sheria.

Amerejelea wasiwasi wake juu ya kuendelea kwa juhudi za kurejesha ukosefu wa utulivi kwenye maeneo mbali mbali nchini CAR.

Bwana Guterres ametoa wito kwa pande kinzani kukomesha ghasia mara moja na kusaka suluhu na kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani.

Katibu Mkuu amerejelea kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia wananchi na serikali ya CAR katika juhudi zao za kusongesha amani na utulivu.

Tukio hilo la kuuawa kwa mlinda amani wa Burundi limekuja siku chache baada ya kuuawa kwa mlinda amani mwingine wa Umoja wa Mataifa kutoka Rwanda nchini CAR.