Tunaendelea kusikitishwa na mauaji na machafuko Tigray:OCHA 

15 Januari 2021

Umoja wa Mataifa umesema unaendelea kusikitishwa na kuendelea kwa taarifa za raia kujeruhiwa na kuuawa kwa raia  wakati wa mapigano yanayoendelea katika maeneo ya vijijini jimboni Tigray nchini Ethiopia na kutiwa hofu kubwa kuhusu janga la maelfu ya watu ambao bado hawajapokea msaada kwenye jimbo hilo kwa zaidi ya miezi miwili na nusu sasa tangu kuzuka kwa machafuko jimboni humo. 

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, ukosefu wa huduma muhimu kama chakula, maji na huduma za afya unaathiri maelfu ya watu, huku wafanyakazi wa shirika hilo walioko kwenye eneo la machafuko wanaripoti kwamba kuna ongezeko la utapiamlo na magonjwa ya mlipuko yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama.

OCHA inasema mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs yamefanikiwa kufikisha msaada katika baadhi ya maeneo na hasa mijini ambako ruhusa ya kuingia katika maeneo hayo imetolewa na serikali. 

Hata hivyo ofisi hiyo imesema idadi ya watu waliofikiwa na msaada ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya watu wanaokadiriwa kuhitaji msaada wa kibinadamu ambao jumla yao ni milioni 2.3. 

Imeongeza kuwa operesheni za misaada ya kibinadamu zinaendelea kukabiliwa na changamoto  ya fursa kamili na huru ya kufikisha misaada hiyo Tigray kwa sababu ya usalama na vikwazo vinavyowekwa na serikali kuu na mamlaka za jimbo hilo. 

“Tumepiga hatua kiasi kwani barabara baina ya Gondar na Shire imeweza kupitika katika siku chache zilizopita na washirika wetu kutoa misaada kwa watu wa Shire kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa machafuko Tigray,"  imesema  OCHA. 

Hata hivyo imesema ucheleweshwaji katika kuidhinisha mchakato huo na haja ya kushirikisha wadau mbalimbali kuingia katika baadhi ya maeneo kunaendelea kuathiri na kuwa kikwazo ya ufikishaji misaada. 

Kwa mantiki hiyo OCHA imesisitiza “Tunarejea wito kwetu kwa pande zote katika mzozo kuruhusu mara moja na kwa usalama wahudumu wa kibinadamu na misaada kuingia Tigray ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuwafikia watu wote wanaohitaji msaada wa kibinadamu.” 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter