Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko nchi jirani na CAR kwa kupokea wakimbizi - UNHCR 

Picha hii kutoka maktaba ikionesha raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) wakivuka mpaka kwa miguu na kuingia Chad.
© IOM/ Craig Murphy
Picha hii kutoka maktaba ikionesha raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) wakivuka mpaka kwa miguu na kuingia Chad.

Heko nchi jirani na CAR kwa kupokea wakimbizi - UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, wakiendelea kumiminika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Chad, Jamhuri ya Congo na Cameroon kufuatia ghasia mpya zilizoibuka nchini mwao, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limepongeza nchi hizo jiranikwa kufungua mipaka yao na kupokea wakimbizi hao. 

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswisi Boris Cheshirkov amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa, “UNHCR inapongeza serikali za nchi jirani kwa kuendelea kuwapatia wakimbizi wa CAR fursa ya ukimbizi kwenye nchi zao na hifadhi licha ya vikwazo vya mpakani vitokanavyo na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.”

UNHCR na wadau wake CAR wamepokea ripoti kuwa vikundi vilivyojihami vinatekeleza vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili wa kingono na uporaji na hivyo inatoa wito kwa pande kinzani kuwa na mazungumzo ya dhati kusongesha amani.

Kwa mantiki hiyo, UNHCR imetoa wito kwa ghasia zikomeshwe CAR kwa kuwa takribani watu 60,000 wamelazimika kukimbilia nchi jirani tangu mwezi Desemba mwaka jana, idadi hiyo ikiwa imeongezeka maradufu katika kipindi cha wiki moja.

Matukio ya mwezi uliopita, tangu kuanza kwa ripoti za ghasia zihusianazo na uchaguzi, yamesababisha kukwama kwa taratibu za wakimbizi wa CAR kurejea nyumbani.

Hivi sasa UNHCR na wadau wake wanaimarisha misaada kwa wakimbizi wapya wanaowasili nchi jirani na CAR licha ya miundombinu duni inayokwamisha utoaji wa huduma za kibinadamu.

Tayari UNHCR imetoa ombi la dola milioni 151.5 kwa mwaka huu ili kukabiliana na operesheni za CAR wakati huu ambapo mahitaji ya wakimbizi wapya nayo yanaongezeka.

Bwana Cheshirkov ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kupanua wigo wa usaidizi wake kwa CAR ili kuwezesha misaada zaidi kufikia watu walio maeneo ya ndani zaidi.