Mama mkimbizi aamua kufa kupona kuitunza familia yake licha ya COVID-19 

13 Januari 2021

Kutana na mkimbizi Fatima, raia wa Syria, na mumewe Abdel Kahar pamoja na watoto wao wadogo wanne ambao wanaishi katika shamba huko Sabha, Mafraq, kaskazini mwa Jordan. Wakati wa ufungaji mipaka kwa sababu ya COVID-19, Fatima hakuweza kufanya kazi shambani hali ambayo ilisababisha kupungua kwa kipato chake cha kawaida.

Huyo ni Fatima Hussein Al Ahmad akieleza alivyotoka Syria akiwa na nduguze. Kwamba walikuja Syria wafanye kazi na pia kukimbia matatizo ya nchi yao. Anasema walianza kufanya kazi. Mwezi huu wakifanya kazi hapa, na mwezi mwingine wakienda katika eneo jingine.  

Fatima na muwewe wanafanya kazi katika shamba wakiokota matunda aina ya fyulisi au ‘peach’ pamoja na nyanya wakiwa na wasyria wengine, watu wa Jordan na pia wahamiaji wengine. 

Anasema ilikuwa vigumu kulazimika kuhama mashamba tofauti kila mwezi. Tulichoka kwasababu ya kuhamahama na pia kukosa makazi, Ilikuwa vigumu, anasema.  

Hatimaye Fatima na familia yake walipewa sehemu ya gari la safari ambalo lina sehemu ya makazi ili waishi humo humo shambani. Maisha yakawa angalau. Lakini hamadi, janga la virusi vya corona likaibuka.  

Anasema, aliacha kufanya kazi na hivyo wakalazimika kukopa pesa kutoka kwa watu ili wakidhi mahitaji kama kumnunulia maziwa bintiye. Tulipita katika wakati mgumu, anaeleza. 

Baadaye Fatima alipambana akaanza kutengeneza jibini na mtindi akiuza katika mji wa Sabha, Mafraq na kisha akipata pesa ananunua maziwa kwa ajili ya mtoto wake mdogo. Anasema miezi ya mwanzoni ya mlipuko wa COVID-19 alipata wakati mgumu sana. Kwanza awapikie watoto wake na kisha wakimaliza kusoma kwa mtandao, akae kuwafundisha.  

Yeye na mumewe walifanya kazi na wengine ili kusaidiana. 

Anasema kuna ushirikiano mkubwa kati yao na majirani zao. Watu wote katika kambi wanasaidiana na wanapeana vitu. Baada ya ile amri ya kutotembea kuondolewa, walifurahi kurejea kazini ili waweze kukidhi mahitaji yao na watoto wao. 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud