Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la kibinadamu linanyemelea Kusini mwa Madagascar wakati COVID-19 na ukame vikiongeza idadi ya walio na njaa-WFP

Mtoto akifanyiwa vipimo vya utapiamlo nchini Madagascar.
WFP/Tsiory Andriantsoarana
Mtoto akifanyiwa vipimo vya utapiamlo nchini Madagascar.

Janga la kibinadamu linanyemelea Kusini mwa Madagascar wakati COVID-19 na ukame vikiongeza idadi ya walio na njaa-WFP

Tabianchi na mazingira

Miaka mitatu mfululizo ya ukame pamoja na kuporomoka kwa uchumi kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona au COVID-19 huenda kukaacha theluthi moja ya wakazi wa kusini mwa Madagascar bila uwezo wa kupata mlo limesema Shirika la Umoja wa Matiafa la mpango wa chakula duniani, WFP. 

Wakati ukame ukishuhudiwa mwaka 2021 na mavuno mabaya, jamii zimeachwa bila raslimali yeyote na wengi wakilazimika kuacha nyumba zao kwend akusaka chakula na ajira. Takriban watu milioni 1.35 wanakadiriwa kukosa uhakika wa chakula hii ikiwa ni asilimia 35 ya watu wote katika eneo hilo. 

WFP imesema janga la ugonjwa wa virusi vya corona au Covid-19 umeongeza madhila na kusababisha ajira nyingi kutoweka na hivyo kuathiri familia zilizokuwa zinategemea vipato hivyo.  

Mwakilishi wa WFP nchini Madagascar Moumini Ouedraogo amesema, “ili kuishi, familia zinakula ukwaju ikiwa imechanganywa na matope,” na kwamba, “hatuwezi kuendelea kwa mwaka mwingine katika hali hii, bila mvua na mazao finyu, watu watakufa kutokana na ukosefu wa chakula. Hakuna mtu anayepaswa kuishi namna hii.” 

WFP imesema watoto ndio waathirika wakubwa wa janga hilo la chakula na wengi wameacha kwenda shule na kuishia mitaaani wakiomba chakula. Utafiti wa WFP umeonyesha kwamba katika eneo la Amboasary mnamo Oktoba 2020 watoto watatu kati ya wane hawahudhuri shule ili wasaidie wazazi wao kusaka chakula. 

Utapiamlo uliokithiri unashuhudiwa miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika maeneo matatu ikiwmeo  Androy, Anôsy na Atsimo Andrefana kwa asilimi 10.7 ikiwa ni kiwango cha pili cha juu katika ukanda wa mashariki na kusini mwa Afrika. 

WFP kwa sasa inato mgao wa chakula kwa takriban watu 500,000 wanaokabilwa na ukosefu wa uhakika wa chakula katika wilay tisa zilizoathirika Zaidi ambapo kulingana na mwenendo hali inaweza kuwa mbaya zaidi ifikapo Juni 2021. 

WFP inatarajia kuimarisha msaada na kufikia watu 900,000 ya watu walio hatarini zaidi. Ili kuendelea na shughuli za kibinadamu WFP, inahitaji dola milioni 35 kwa ajili ya mgao wa chakula na pesa taslimu na programu za utapiamlo. Aidha inahitaji fedha kwa ajili ya mlo shuleni kuhakikisha watoto wanasalia shuleni ili kuwajengea mustakabali bora.