Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

AFIKEPO yashamirisha afya za watoto Malawi 

Familia ikipata mlo wao wa kila siku nyumbani kwao wilaya ya Balaka nchini Malawi (Juni 2016)
UNICEF/Sebastian Rich
Familia ikipata mlo wao wa kila siku nyumbani kwao wilaya ya Balaka nchini Malawi (Juni 2016)

AFIKEPO yashamirisha afya za watoto Malawi 

Utamaduni na Elimu

Nchini Malawi mradi wa kuboresha lishe kwa watoto unaotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na mdau Muungano wa Ulaya, umeleta matumaini makubwa kwa wazazi ambao watoto wao awali walikumbwa na udumavu uliotia mashaka uhai wao.

Elenesi Pagambo, mmoja wa wahamaishaji wa mradi wa AFIKEPO akisema kuwa ujio wa mradi huo umeleta maendeleo makubwa. Hivi sasa wana bustani za mboga za majani, wanafuga kuku, halikadhalika mabanda bora ya kufugia mbuzi na zaidi ya yote wana chakula bora kwa watoto wao. 

 Verita Tengani akiwa na mwanae anasema “umenikuta hapa namlisha mwanangu mlo wa mchana. Mwanangu alizaliwa njiti, uzito wake ulikuwa mdogo mno, kilo 1 na gramu 300. Mwanzoni nilihofia sana nikadhani mwanangu atakufa. Mlo huu una aina nne za vyakula. Mboga za majani kuzuia magonjwa. Chakula kinasaidia mwanangu awe na afya nzuri.” 

Anasema gari la mradi wa AFIKEPO nalo hupita kijijini na kuwashauri wao na watoto wao kunawa mikono kwa maji na sabuni. 

Mradi wa AFIKEPO unaotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la kuhudumia watoto, UNICEF, na la chakula na kilimo FAO na mdau EU,  pamoja na masuala ya lishe, unahamasisha ushiriki wa baba kwenye malezi ya mtoto. 

Nats.. 

Baba huyu anasema mwanae anapougua naye anashiriki kumpeleka hospitali na zaidi ya yote anahakikisha wana mlo kamilifu na wa kutosha. 

Nats.. 

Kupitia wahamasishaji wa mpango huu, vikundi hukutana na kuoneshwa jinsi ya mapishi ya aina aina mbali mbali za vyakula ikiwemo wanga, protini na mboga za majani. 

Unga wa mahindi unatumika kupika ugali ambao hujenga mwili, huku mboga za majani zikichanganywa na karanga na nyanya ili kulinda mwili. 

Nats.. 

Na hatimaye ni matunda kama vile maembe, bila kusahau mayai ambayo wanakikundi wanajulishwa kuwa yana protini za kutosha. 

Mhamasishaji anawajulisha kuwa vyakula hivyo vyote ni bora kwake yeye ambaye ni mjamzito na pia mwanae aliye tumboni.