Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuko kwenye mawasiliano na mataifa yote ambayo yako katika mchakato wa utengezaji chanjo za COVID-19-WHO 

Chuo cha Oxford kilitangaza kwamba wanasayansi wamebuni chanjo dhidi ya COVID-19.
University of Oxford/John Cairns
Chuo cha Oxford kilitangaza kwamba wanasayansi wamebuni chanjo dhidi ya COVID-19.

Tuko kwenye mawasiliano na mataifa yote ambayo yako katika mchakato wa utengezaji chanjo za COVID-19-WHO 

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Dkt Tedros Gebreyesus akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi ametoa wito kwa nchi zote kutekeleza ahadi zao katika kuwezesha upatikanaji wa chanjo dhidi ya virusi vya corona. 

Dkt Tedros amesema, “wiki ijayo katika Bodi ya Utendaji ya WHO, nitahimiza nchi zote kutimiza ahadi zao kwa COVAX.” 

COVAX ilianzishwa na WHO ili inashughulika na kuhakikisha chanjo inapatikana kwa watu wote ulimwenguni.   

Mkuu huyo wa WHO amesema anatoa wito wa kujitolea kwa pamoja ili ndani ya siku 100 zijazo, chanjo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na walio katika hatari kubwa kwenye nchi zote ziendelee.  

Aidha Gebeyesus amesema serikali, wazalishaji, asasi za kiraia, viongozi wa kidini na jamii lazima wajiunge pamoja kuunda uhamasishaji mkubwa zaidi katika historia ya chanjo na kwamba WHO inaendelea kuomba watengenezaji wa chanjo kutoka kote ulimwenguni kwenda haraka kutoa data zote muhimu zinazohitajika ambazo zitairuhusu WHO kuzizingatia kwa ajili ya kuziorodhesha chanjo hizo katika matumizi.  

 “Nimefurahi kuwa timu ya WHO iko nchini China hivi sasa inafanya kazi na wazalishaji wa chanjo za Sinovac na Sinopharm kutathmini uzingatiaji wa viwango vya utengenezaji wa ubora wa kimataifa kabla kuorodheshwa kidharura katika matumizi ambako kunafanywa na WHO.” Amedokeza Dkt Gebreyesus. 

Pia Mkuu huyo wa WHO amesema wanatarajia pia Taasisi ya Serum ya India kuwasilisha seti kamili za data kwa ajili ya tathmini ya haraka ili WHO iamue ikiwa wanaweza kupendekeza chanjo yao ya AstraZeneca kwa matumizi ya kimataifa. 

“Hii ni mifano michache tu ya kazi inayoendelea kwa WHO, GAVI, CEPI na wadau  wengine wenye lengo la ugawaji salama wa chanjo salama, haraka, usambazaji kwa busara na usawa.” Ameeleza Tedros.  

Akikisisitiza kuhusu ushirikiano, Dkt Tedros amesema, “kama ambavyo nilisema awali na nitasema tena. Kuokoa maisha, ustawi na uchumi kunategemea katika makubaliano ya ulimwengu ili kukwepa chanjo kutolewa kwa kuzingatia utaifa.”