Mwaka 2021 lazima uwe wa maridhiano baina ya sayari dunia na mazingira

11 Januari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mwaka huu utakuwa muhimu sio tu kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona, COVID-19 lakini katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kwenye mkutano wa 26 wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP26, kikao cha Afrika, mabadiliko kuelekea nishati safi kilichofanyika kwa njia ya mtandao, Katibu Mkuu amesema lengo kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu ni kujenga muungano wa dunia nzima kwa ajili ya kumaliza matumizi ya gesi ya mkaa ifikapo katikati mwa karne hii. 

Bwana Guteress amesema Uingereza kama mwenyeji ina jukumu kubwa na kwamba, “kufikia kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050, tunahitaji kuachana na matumizi ya mafuta kisukuku na kugeukia mafuta yanayojali mazingira na tunahitaji kuunga mkono nchi zinazoendelea katika hili na kwa hiyo ninakaribisha majadiliano ya leo yakilenga Afrika.” Ameongeza kwamba katika hilo kuna malengo mawili. ujumuishwaji na uendelevu. Takriban watu milioni 789 wanaoishi katika nchi zinazoendelea hawana umeme kabisa. 

Katibu Mkuu ameongeza kusema, “robo tatu ya watu hawa wanaishi Kusini mwa Jangwa la Sahara.Hii ni dhuluma na kikwazo kwa maendeleo endelevu.Mataifa yote yanahitaji kutoa upatikanaji wa umeme kwa wote. Lakini kawi hiyo inahitaji kuwa isiyochafua mazingira na endelevu ili isichangie katika kuongeza nyuzi joto kwenye sayari na hiyo inamaanisha dhamira thabiti kutoka kwa serikali zote."

Bwana Guterres amerejelea wito wake kwa nchi zilizoendelea kutimiza ahadi yao ya dola bilioni 1000 kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea kuzuia na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ameongeza kwamba, “ Benki ya Dunia na benki ya maendeleo Afrika na benki za maendeleo kitaifa ni lazima zibuni vifaa vya kuwekeza ambavyo vitapunguza hatari ya kuwekeza na kuvutia uwekezaji binafsi kutoka nchi za Afrika." 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba tayari tunashuhudia athari za mabadiliko ya tabianchi na kwa hiyo ni muhimu tusipuuuze umuhimu wa marekebisho, na kwamba, uhatari wa Afrika ni dhahiri, kuanzia ukame wa muda mrefu Sahel na Pembe ya Afrika na mafuriko kusini mwa Afrika. Marekebisho ni suala la kimaadili na haipaswi kusahaulika katika hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 

Ameongeza kwamba kongamano la Januari 25 ni fursa ya kuchagiza hatua kuhusu eneo hilo lililosahaulika. 

Bwana Guterres akizungumzia ufadhili kwa ajili ya kuibuka kutoka COVID-19 amesema uwekezaji endelevu haujapewa kipaumblele na kwamba, “ni lazima tuwekeze katika mustkabali wa nishati endelevu kwa ajili ya watu wote popote walipo hususan Afrika." Aidha ameongeza, “cha msingi ni kwamba fedha za umma na za sekta binafsi zinapaswa kuunga mkono malengo ya mkataba wa Pari na Ajenda 2030 ya maendeleo endelevu. Ninatoa wito hususan kwa sekta binafsi wachagizaji wa nishati endelevu."

Katibu Mkuu Guterres amesema wakati wengi wanajenga mitandao mashinani, kitaifa na kimataifa tunahitaji ujuzi wao na ubunifu katika kufikia mabadiliko kwa haraka ya nishati endelevu na kwamba mabadiliko hayo yanahitaji kuwa yenye haki na jumuishi, “hii inamaanisha kutoa mafunzo na stadi mpya na kutoa fursa mpya. 

Kwa kuhitimisha Katibu Mkuu amesema, “tunayo fursa ya kubadili dunia, lakini ili kufanya hivyo tunahitaji ushirikiano wa kimataifa, kama ilivyo kwa ajili ya kuibuka kutoka kwa COVID-19. Afrika ni lazima iwe katikati ya majadiliano. Wakati wa janga la ulimwengu tunajilinda vizuri tunapowalinda wote. Tuna vifaa. Hebu na tuzitumize kupitia dhamira ya kisiasa.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud