Mradi wa kuboresha mazingira Sahel GGW wapigwa jeki ya dola zaidi ya bilioni 14

11 Januari 2021

Mradi kabambe wa kukabiliana na hali ya jangwa kwenye ukanda wa sahel na Sahara wa Great Green Wall, GGW  umepokea ufadhili wa dola bilioni 14.236 za kimarekani. 

Ufadhili huo umetangazwa leo kupitia taarifa iliyotolewa Bonn, Ujerumani na Paris, Ufaransa, na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika kongamano la sayari moja linalofanyika kwa njia ya mtandao likijikita na masuala ya bayoanuai ambalo limeratibiwa na Ufaransa, Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia. 

Ufadhili huo utasaidia kuchagiza hatua za kurutubisha ardhi, kuokoa bayoanuai, kukuza kazi zinazojali mazingira na kuwajengea mnepo watu wa ukanda wa Sahel. 

Ukuta huo wa GGW unapitia jangwa la Sahara maeneo ya kusini kutoka  pwani ya Atlantiki hadi baharí ya Shamu. Ufadhili wa leo ni asilimia 30 ya dola bilioni 33 za kimarekani zinazohitajika kutimiza malengo yake ifikapo mwaka 2030. 

Rais wa Mauritania Mohamed Cheikh El-Ghazouani, ambaye ni mwenyekiti wa kongamano la viongozi wa nchi na serikali wa kusimamia GGW amekaribisha mpango huo kwa niaba ya ukanda akisema, “tunakaribisha kutangazwa kwa mradi wa haraka wa Great Green Wall ambao lengo lake ni kutoa ufadhili wa kwanza katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 ili kuhakikisha kutekelezwa kwa dhamira ya wadau wa kifedha katika utaratibu unaofaa.’ 

Rais Ghazouani ameongeza kwamba, “uchangishaji wa fedha zingine kupitia njia bunifu utasaidia kufikia malengo ya Great Green Wall ambao unalenga kurekebisha hekari milioni 1000 zilizoharibiwa na kubuni ajira  milioni 1o zinazojali mazingira..” 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress amesema, kwa kupanda mimea hekari milioni 100 zilizoharibiwa, uhakika wa chakula utahakikishwa, kaya zitabaki na ajira kubuniwa. Ameongeza kwamba juhuzi hizo zitarjesha bayoanuai, kupunguza makali ya mabadiliko ya tabianchi na kujengea jamii mnepo. 
 
Rais Ghazouani amesisitiza kwamba ufadhii huo, “utasaidia nchi zetu katika kufikia fedha zinazohitajika kwa ajili ya kuimarisha ufadhili mashinani ndani ya muongozo wa mambo matano yaliyopitishwa na kuimarisha uwezo wa mashirika ya kitaifa kwa ajili ya Great Green Wall. Kwa mantiki hiyo ningependa kupendekeza kuanzishwa katika kila nchi mfuko wa bayoanuai ambao tutatoa sehemu ya raslimali zitokanazo na kufutwa kwa deni zetu. Kufutwa ambako tunaomba kutoka mioyo yetu.” 
 
Tangu kuanzishwa kwa mradi wa Great Green Wall mwaka 2007 umeungana na wadau wengi kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ukanda huo na kujenga kilometa 8000 za msitu katika nchi takriban 11 na kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo waka 2030. 

Mradi huo ambao sasa uko katika muongo wa pili ni kielelezo cha kutumia nguvu asilia kwa ajili ya kutoa suluhu za kimazingira kama vile kuharibiwa kwa mazingira, kukua kwa jangwa, ukame, mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa bayoanuai, umaskini na ukosefu wa uhakika wa chakula. 
 
Kongamano linakusanya raslimali, viongozi wa serikali na wadau ikiwemo viongozi kutoka mashirika ya kimataifa, taasisi za kifedha, sekta ya biashara na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ajili ya kukubaliana kuchukua hatua Madhubuti kulinda bayoanuai na kutangaza upya na kuzindua mikakati itakayoleta mabadiliko kwa ajili ya mazingira. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter