Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninalaani kitendo hiki cha kutisha, kilichoua na kujeruhi watoto-Henretta Fore 

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, Henrietta Fore akiwa ziarani Mali
UNICEF/Keïta
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, Henrietta Fore akiwa ziarani Mali

Ninalaani kitendo hiki cha kutisha, kilichoua na kujeruhi watoto-Henretta Fore 

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mtaifa la kuhudumia watoto UNICEF, Henrietta Fore  amelaani vikali shambulizi ambalo limetekelezwa jana na kuua wananchi wakiwemo watoto katika mji wa Mozogo, kaskazini mwa Cameroon. 

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo Dakar, Senegal na New York Marekani, shambulizi hilo lenye nia ya kujiua na kuua wengine, limesababisha vifo vya watu 15 wakiwemo watoto watano wenye umri kati ya miaka 3 na 14 huku wengine sita wenye umri wa miaka 9 na 16 wakijeruhiwa sana.  

Bi. Fore amesema, “ninalaani kitendo hiki cha kutisha na ninatoa wito wa kukomeshwa kwa mashambulizi dhidi ya watoto, familia na jamii. Hakuna kabisa haki ya kuwalenga au kuwatumia watoto kutekeleza mashambulizi.”   

Aidha Bi. Fore amesema anaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa idadi ya mashambulio dhidi ya raia katika maeneo ya Kaskazini, Kaskazini Magharibi na Kusini-Magharibi mwa Cameroon. Kuongezeka kwa vurugu kumezidisha mzozo wa kitaifa wa kibinadamu na sasa kuna takriban watoto milioni 3.2 wenye uhitaji kote Cameroon. 

"Hali kwa watoto na familia zilizo katika mazingira magumu zimekuwa mbaya zaidi kutokana na  kufungwa kwa shule nyingi, milipuko ya magonjwa na matokeo ya kiuchumi na kijamii ya janga la COVID-19. UNICEF inaendelea kufanya kazi na Serikali na wadau wetu katika jamii zilizoathiriwa kuwapa watoto na familia ulinzi muhimu, huduma za afya na huduma za elimu, lakini hii haitoshi. Msaada wa ziada na ushiriki kutoka kwa jamii ya kimataifa unahitajika haraka kutusaidia kufikia wale ambao wanahitaji zaidi.” Amesema Bi. Fore.