Kanuni za kudhibiti COVID-19 Uganda zisitumike kubinya uhuru wa kukusanyika

8 Januari 2021

Ofisi ya haki za binadamu ya  Umoja wa Mataifa, OHCHR, imeeleza wasiwasi wake juu ya kuendelea kuzorota kwa haki za binadamu nchini Uganda wakati huu ambapo taifa hilo linajianda kwa uchaguzi  mkuu tarehe 14 mwezi huu wa Januari.

Msemaji wa ofisi hiyo Ravina Shamdasani amewaambia waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi kuwa hofu yao ni kwamba mazingira ya sasa yanaweza kuleta changamoto siyo tu wakati wa uchaguzi bali pia hata baada ya uchaguzi mkuu.

Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyoripotiwa ni pamoja na kubinywa kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani na watu kukamatwa na kuswekwa rumande kiholela. Ameenda mbali zaidi akisema kuwa, “kati ya tarehe 18 na 20 Novemba 2020, takribani watu 54 waliuawa wakati wa maandamanao kwenye wiaya 7 nchini Uganda kufuatia kukamatwa na kuwekwa ndani kwa wagombea wawili wa kiti cha uraia, Robert Kyagulanyi, al maaruf Bobi Wine na Patrick Oboi Amuriat, pamoja na wanachama wa chama cha upinzani. “

Waandishi wa habari waliokuwa wanaandika habari za mkutano huo wa kampeni wa Amuriat, yaripotiwa walipigwa na vikosi vya usalama na kuamriwa kufuta picha na video ambazo walikuwa wamechukua wakati wa mkutano huo wa kampeni- Ravina Shamdasani, Msemaji OHCHR

Halikadhalika amesema kunafanyika manyanyaso, uonevu na kuwekwa ndani kwa wafuasi wa vyama vya upinzani, ambapo Kyagulanyi, ambaye ni mgombea urais kupitia chama cha National Unity Platform (NUP), amezuiwa kufanya kampeni za uchaguzi mara kadhaa.

Ametaja matukio mengine ya karibuni kuwa ni pamoja na Oboi Amuriat, mgombea urais kupitia chama cha Forum for Democratic Change (FDC), kukamatwa tarehe 2 mwezi huu wa Januari wakati akifanya kamepni kwenye wilaya ya Nakasongola na baadaye kuachiwa huru kwa dhamana.

Waandishi wa habari waliokuwa wanaandika habari za mkutano huo wa kampeni wa Amuriat, yaripotiwa walipigwa na vikosi vya usalama na kuamriwa kufuta picha na video ambazo walikuwa wamechukua wakati wa mkutano huo wa kampeni.

Akihusisha kanuni za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Corona au COVID-19 wakati wa kampeni za uchaguzi, Bi. Shamdasani amesema sheria za haki za binadamu katika mazingira fulani zinaweza kuruhusu vikwazo vya mikusanyiko ya watu wengi na kampeni kwa sababu za kiafya. “Hata hivyo tumeendelea kubaini kuwa vikwazo dhidi ya COVID-19 vimekuwa vikifuatiliwa zaidi kwenye maeneo ya kampeni za vyama vya upinzani kwa mtindo wa kibaguzi.”

Ametoa mfano taree 30 mwezi uliopita wa Desemba mwaka 2020 ambapo wafuasi 90 wa chama cha NUO walikamatwa huko Kalangala wakati vikosi vya usalama vilivpozuia kampeni ya Bwana Kyagulanyi kwa madai ya kukiuka kanuni za kudhibiti kuenea kwa COVID-19.

Msemaji huyo wa OHCHR ametamatisha mkutano wake na waandishi wa habari akisema, “tunatoa wito kwa mamlaka za Uganda zilinde haki za uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, na kuhakikisha mchakato huru na haki wa uchaguzi ambao unatoa hakikisho la wananchi wa Uganda kushiriki katika masuala yao ya kiraia, ikiwemo kuchukua hatua kuzuia matukio ya ghasia wakati wa uchaguzi.”

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter