Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wawaaga kwa heshima walinda amani waliopoteza maisha CAR 

Umoja wa Mataifa wawaaga kwa heshima walinda amani waliopoteza maisha CAR
MINUSCA
Umoja wa Mataifa wawaaga kwa heshima walinda amani waliopoteza maisha CAR

Umoja wa Mataifa wawaaga kwa heshima walinda amani waliopoteza maisha CAR 

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa kupitia mpango wake wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA umewaaga kwa heshima  walinda amani kutoka Burundi, Bangladesh, na Cameroon ambao walipoteza maisha yao hivi karibuni wakiwa kazini.

Katika Makao Makuu ya MINUSCA mjini Bangui, walinda amani katika mwendo wa taratibu wanajongea wakiwa wamebeba majeneza ya wenzao. Majeneza yamefunikwa bendera ya Umoja wa Mataifa pamoja na bendera za nchi wanakotoka, askari waliopoteza maisha.  

Siku ya sikukuu ya Christmas, usiku, walinda amani watatu wa Burundi waliuawa wakiwa katika jukumu la kulinda raia dhidi ya shambulio la vikundi vyenye silaha huko Dekoa. Kesho yake ilikuwa siku ya  kuamkia uchaguzi wa rais na wabunge nchini humo Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mlinda amani wa kutoka Cameroon yeye aliuawa katika ajali ya barabarani wakati wa usindikizaji wa kawaida, huku mlinda amani wa Bangladesh akipoteza maisha baada ya kuugua kwa muda mfupi.  

(Nats) 

Huyo ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, Bwana Mankeur Ndiaye anasema, "ninataka kukumbushia kwamba wanaume hawa watano mashujaa  walikufa ili moto wa matumaini na amani uwake katika nchi ya Afrika ya Kati. Walikufa ili watu wa Afrika ya Kati waweze kuishi kwa usalama na hadhi, waweze kutekeleza jukumu lao la kiraia kupiga kura katika mazingira hatari sana, yenye hali mbaya, iliyozidishwa na janga la COVID-19 licha ya udhaifu wa kiuchumi na kiafya ambao bado unakumba Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wamelipa bei ya kujitolea kwao na kwa ubora tunaoshiriki wote. Kuifanya dunia hii, nchi hii kuwa mahali pazuri.” 

Kamanda Mkuu wa Kikosi cha MINUSCA Daniel Sidiki Traoré amewasifu walinda amani wa Burundi walioofariki dunia kama askari hodari ambao wametoa sadaka kuu ya kutoa maisha yao kuokoa maisha ya wengine kwa jina la amani. 

(Nats) 

Kamanda Traoré anasema, "ijapokuwa ni wakati wa huzuni, tunaona ni busara kuheshimu na kusherehekea ukuu wao na kujitolea kwao kwa njia ya jukumu na huduma kwa wanadamu." 

Mwisho wa tukio hilo la kuaga, miili ya walinda amani wa Burundi imerejeshwa Bunjumbura, baada ya MINUSCA kupata heshima za kijeshi kwenye Uwanja wa ndege wa Bangui Mpoko mbele ya Mkuu wa Kikosi, ambaye alikabidi barua ya rambirambi kwa kamanda wa kikosi cha Warundi. Walinda amani wote watano wamepewa tuzo ya heshima ya juu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.