Lishe ya WFP iliniokoa, sasa natumikia WFP kusaidia wengine- Liberee Kayumba

6 Januari 2021

Wahenga walinena ukishikwa shikamana, na ndivyo anavyofanya Liberee Kayumba ambaye ni manusura wa mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi yaliyofanyika mwaka 1994, anasema yuko hai leo hii sababu ya msaada wa chakula wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP , ambao ulimuhamasisha baadaye kujiunga na shirika hilo kusaidia wakimbizi wa Burundi kama alivyosaidiwa.

Liberee ameshuhudia madhila ya vita kwa macho yake, kwani alipokuwa na umri wa miaka 12 tu alipopoteza wazazi wake wote na kaka zake kwenye mauaji  ya kimbari na kuwa kwenye hatari kubwa ya kufa njaa.  Anasema “Kwa miezi mitatu nilikuwa ndani tu ya nyumba bila kujua kama ntaishi ama nitakufa saa yoyote, hakuna hata mtu mmoja kwenye familia aliyeweza kutoka nje wakati huo kwenda kufanya kazi au kulima hivyo kupata chakula ilikuwa vigumu, tusingeweza kuishi bila msaada wa kibinadamu wa chakula wa WFP 

Na msaada huo ndio uliokuwa hamasa kwake kujiunga na WFP ili asaidie kuleta mabadiliko kwenye maisha ya wengine wanaopitia madhila aliyowahi kuyaonja. 

Hivi sasa ni afisa mwangalizi wa WFP kwenye kambi ya wakimbizi ya Mahama, iliyoko kilometa chache kutoka mpaka wa Tanzania ambayo inatoa msaada wa mgao wa chakula kila mwezi kwa karibu wakimbizi 60,000 wa Burundi. 

Liberee anaongeza kuwa “tangu nilipokuwa mtoto nilipenda kusaidia wenye uhitaji, inakutia moyo kufanya hivyo unaposhuhudia watu wakiua watu wengine na madhila yote yanayotokea. Kumbukumbu za mauaji hayo na watu wote wanaohitaji msaada ndio vimenihamasisha kujiunga na WFP” 

Kwa Liberee sio tu anahisi uchungu wa madhila ya wakimbizi bali pia anaelewa jukumu kubwa la chakula kwa jamii zilizo hatarini zinazokimbia vita. 

Na anasema asilani hatosahau msaada wa chakula waliopewa na WFP wakati huo ambao uliokoa maisha yake na ya maelfu ya Wanyarwanda wengine. Na anaamini kwamba sasa “dunia nzima inaelewa kwamba msaada wa kibinadamu wa chakula ni muhimu sio tu kwenye vita na majanga bali pia katika kushirikiana na serikali zote duniani katika kufikia lengo la kutokomeza njaa.” 

WFP bado inaendelea kutoa mgao wa chakula kwa takriban wakimbizi 138,000 kutoka nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter