UNHCR inaendela kupokea na kuandikisha wakimbizi kutoka Ethiopia wanaoingia Sudan

5 Januari 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linaendelea kuandikisha wakimbizi wapya katika mpaka wa Sudan na Ethiopia ambapo takriban wakimbizi 800 wamevuka kutoka eneo la Tigray nchini Ethiopia na kuingia mashariki mwa Sudan katika siku chache za mwaka huu wa 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu, mjini Geneva Uswis, msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic amesema tangu Novemba mwaka jana, zaidi ya wakimbizi 56,000 kutoka Ethiopia wamefungasha virago kukimbia machafuko  na kuingia nchi jirani Sudan na kwamba,“Wanaowasili wanaelezea kuwa katikati ya mzozo na kuwa waathirika wa makundi kadhaa yaliyojihami huku wakikabiliwa na hali ngumu ikiwemo, uporaji wa nyumba zao, kutumikishwa kwa lazima kwa wanaume na wavulana, na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana.” 

UNHCR imesema wakimbizi wanaowasili wanafika na nguo tu walizovaa, wakiwa wamechoka na wakiwa dhaifu baada ya safari ya siku nyingi. Asilimia 30 ya  wakimbizi wanatajwa kuwa chini ya umri wa miaka 18 na asilimia 5 wana umri wa zaidi ya miaka 60. 

Bwana Mahecic ameongeza kwamba kwa kushirikiana na serikali ya Sudan, UNHCR na kamisheni ya wakimbizi Sudan, COR wanaendelea kuhamisha wakimbizi kutoka kwenye maeneo ya mapokezi ambayo yamejaa hadi kwenye kambi zilizoko jimbo la Gedaref. Aidha amesema mahitaji ya wakimbizi ni mengi na kwamba,“Serikali ya Sudan inaendelea kuacha mipaka yake wazi kwa ajili ya wakimbizi lakini msaada zaidi unahitajika hususan kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji na kujisafi kwenye kambi na maeneo ya mapokezi. Pia kuimarisha mbinu za kuzuia Covid-19 ikiwemo kujitenga.” 

 Kufikia mwisho wa mwaka 2020 dola milioni 40 zilikuwa zimeahidiwa kwa UNHCR kwa ajili ya dharura eneo la Tigray ambazo ni sawa na asilimia 37 ya mahitaji ya kifedha yanayohitajika nchini Sudan, Ethiopia na Djibouti.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter