Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya nukta nundu yasisitiza umuhimu wa kufikia taarifa

Mtoto akisoma nukta nundu shuleni nchini Uganda
UNICEF/Michele Sibiloni
Mtoto akisoma nukta nundu shuleni nchini Uganda

Siku ya nukta nundu yasisitiza umuhimu wa kufikia taarifa

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa unaadhimisha siku ya nukta nundu duniani Jumatatu Januari 4, kwa kusisitiza umuhimu wa mfumo huu wa kupitisha habari kwa ajili ya kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu wa kutoona na watu wenye uoni hafifu

Watu wenye ulemavu wa kutoona wako hatarini ya kukabiliwa na viwango vya juu vya umasikini, kutengwa na ukatili. Janga la corona na athari zake, kwa mfano vikwazo, vimeongeza changamoto za kundi hilo na kuwatenganisha zaidi watu hawa.
Kwa mujibu wa Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO takriban watu bilioni 2.2 duniani kote wana ulemavu wa kutoona ambao kati yao hao bilioni 1 wana ulemavu wa kutoona ambao ungezuilika au ambao unaweza kutibiwa.


Nukta nundu na COVID-19

Janga la corona limedhihirisha umuhimu wa kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa njia inayoweza kufikiwa ikiwemo nukta nundu na mfumo wa sauti kuhakikisha kwamba kila mtu anafikia taarifa muhimu kwa ajili ya kujilinda na kusaidia kupunguza kuenea kwa COVID-19

Umoja wa Mataifa, kwa upande wake umeweka mikakati mizuri kwa ajili ya kuimarisha ujumuishwaji wa wote vita dhidi ya COVID-19.
Nchini Malawi, kwa mfano Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP lilichapisha nakala 4,050 za nukta nundu kwa ajili ya kuimarisha uelewa kuhusu COVD-19, wakati nchini Ethiopia, Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, OHCHR imetoa taarifa kupitia mfumo wa sauti na elimu na vifaa vya mawasiliano kwa waandishi habari na kutengeneza pia nakala za nukta nundu.
Kwa upande wake Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF lilitoa muongozo katika lugha mbali mbali na mifumo inayofikika ikiwemo nukta nundu kuhusu mambo ya kuzingatia kwa watoto na watu wazima walio na ulemwavu katika kukabiliana na COVID-19

Kuhusu siku hii ya kimataifa 
 

Siku ya nukta nundu duniani huadhimishwa kila Januari 4 baada ya kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 2018. Tarehe hiyo inalingana na kuzaliwa kwa Louis Braille, ambaye akiwa na umri wa miaka 15, alizindua mfumo wa kusoma na kuandika wa nukta nundu kwa ajili ya matumizi na watu wenye ulemavu wa kutoona au uoni hafifu.
Nukta nundu husomwa kwa kupitisha ncha ya vidole juu ya nukta kati ya moja hadi sita zilizochorwa, ambazo zinawakilisha herufi, nambari pamoja na alama za muziki na hisabati. Nukta nundu inaweza kuandikwa kwa kutumia mashine na nukta nundu au kwa kutumia kalamu maalum na kitabu cha nukta nundu kuweka shimo kwenye karatasi.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, CRPD unataja mfumo wa nukta nundu kama njia ya mawasiliano na inataja kama muhimu katika elimu, uhuru wa kujieleza na kupata taarifa na ujumuishwaji katika jamii, kwa watumiaji wake.
Mfumo wa nukta nundu umerekebishwa katika kipindi cha miaka mingi kuanzi 1949 ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni lilichukua jukumua la utafiti ukilenga kuonisha mfumo wa nukta nundu.