Buriani  Sir Brian Urquhart umeacha mchango mkubwa UN na duniani:Guterres

3 Januari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelrezea huzuni yake kufuatia kifo cha afisa wa zamani wa ngazi ya juu kwenye umoja wa Mataifa Brian Urquhart aliyeutumikia Umoja wa Mataifa kwa miaka zaidi ya 40.

Antonio Guterres kupiotia ujumbe wake uliotolewa leo na msemaji wake ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Sir Brian na wote waliompenda ndani nan je ya Umoja wa Mataifa.
Sir Brian aliyekuwa aliyepigana vita vya pili vya dunia, alikuwa mtu wa pili kuajiriwa kwenye Umoja wa Mataifa na alifanyakazi kwa karibu na makatibu wakuu watano wa zamani wa Umoja wa Mataifa akishjikilia nyadhifa mbalimbali ikiwemo kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu kwa ajili ya masuala ya kisiasa.
Katika taarifa hiyo Bwana Guterres amesema “Urquhart ambaye alitimiza miaka 101 aliweka kiwango cha mtumishi wa umma wa kimataifa kwa kujitolea na kutopendelea.”

Mchango wa Brian Urquhart

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya Habari Katibu Mkuu ameongeza kuwa kama msaidizi wa Katibu Mkuu wa zamani Dag Hammarskjöld, Urquhart alisaidia kufafanua wigo wa kazi za Umoja wa Mataifa katika kushughulikia mizozo ya silaha na changamoto zingine za kimataifa.

Na wakati akiwa msaidizi wa karibu wa afisa muhimu mshauri wa Umoja wa Mataifa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Ralph Bunche, Sir Brian alisaidia kuanzisha operesheni za kimataifa za kulinda amani na kisha na kuzisukuma kutumika kwa kiasi kikubwa.

Kwa miongo kadhaa na kupitia kazi yake na makatibu wakuu mbalimbali wa Umoja wa Mataifa Bwana. Brian amekuwa kitovu cha matukio mbalimbali ya kimataifa kuanzia Congo hadi Mashariki ya Kati.

Tutakuenzi daima kwa uliyofanya

Kwa mujibu wa Bwana. Guterres ushiriki wa Brian katika masuala ya kimataifa uliendelea hata alipostaafu kazi kwenye Umoja wa Mataifa kupitia uandishi wake ambao ulijumuisha wasifu wa Dag Hammarskjöld, na Bench.

Pia alikuwa kioo na mwalimu bora kwa wafanyakazi wa umoja wa Mataifa na vijana wengi sana katika safari zao za ajira.

Kitabu cha Maisha ya Urquhart alichokiita “A life in Peace and War”akimaanisha Maisha katika amani na vita kikielezea siku za mwazo aza Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu amesema kinatoa matumaini kwa kila mtyu kuamini kwamba kuna uwezekano wa kujenga dunia yenye amani na haki.

Ameongeza kuwa katika Maisha yake yote Brian Urquhart ni mtu wa matumaini ambayo yameujenga Umoja wa Mataifa na kuandika historia.

Guterres amehitimisha taarifa yake kwa kushukuru mchango mkubwa alioutoa Urquhart akihudumu kwenye Umoja wa Mataifa kwa dunia nzima.

Mpaka alipostaafu mwaka 1986 mbali ya kuwa mshauri mkuu kwa Makatibu wakuu watano wa Umoja wa Mataifa , aliongoza operesheni 13 za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, aliajiri wanajeshi 10,000 kutoka nchi 23 na alifanya operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa kuwa ni kitovu cha shirika hili la kimataifa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter