Kundi la mwisho 2020 la waomba hifadhi kutoka Libya limeondoka kuelekea Rwanda :UNHCR

30 Disemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limefanikiwa kulihamisha kundi la waomba hifadhi 130 waliokuwa hatarini nchini Libya na kuwapeleka kwenye usalama nchini Rwanda, katika awamu ya nne na ya mwisho ya mwisho kwa mwaka huu wa 2020.

Kwa mujibu wa UNHCR Ndege zingine za kuwahamisha waomba hifadhi hao zitaanza tena mwaka 2021.

Ndege hiyo iliondoka jana Jumanne mchana mjini Tripoli kuelekea uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Kigali Rwanda ambako leo wafanyakazi wa UNHCR na mamlaka ya Rwanda wamewapokea na kuwakaribisha waomba hifadhi hao.

Kundi la wahamiaji hao linajumuisha wanaumme, wanawake na watoto kutoka Eritrea, Sudan, Ethiopia na Somalia.

Na wengi wa waoomba hifadhi hawa walikuwa wanaishi maeneo ya mijini hasa Tripoli na wengi walikuwa wameshikiliwa rumande siku za nyuma katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo.

Jean-Paul Cavalieri mkuu wa UNHCR nchini Libya amesema“Kitendo cha kuwahamisha watu hao kupitia mpango wa ETM kumedhihirisha kuwa ni hatua muhimu ya kuokoa Maisha kwa wakimbizi na waomba hifadhi nchini Libya na juhudi zaidi ni lazima ziweke na jumuiya ya kimataifa ili kutoa msaada mkubwa zaidi kwa watu hawa.”

Kundi la baadhi ya wakimbizi 116 ambao wamewasili katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali kufuatia kuhamishwa nchini Libya.
©UNHCR/Eugene Sibomana
Kundi la baadhi ya wakimbizi 116 ambao wamewasili katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali kufuatia kuhamishwa nchini Libya.

Ameongeza kuwa “ Kwa wakimbizi nchini Libya janga la COVID-19 sio tu kwamba limewapa vikwazo ambavyo vimewasababishia kupoteza uwezo wa kuishi , uhakika wa chakula na kukosa fursa za huduma za afya lakini pia limeathiri fursa zao za kupata njia ya kisheria na suluhu za kutoka nchini Libya, na hivyo kuwaongezea hamaki wale waliohatarini zaidi. Hivyo tunaziomba nchi zinazowapokea kuwapa fursa zaidi za Maisha ili kutusaidia tuweze kuwahamisha waomba hifadhi zaidi walio kwenye hatari nje ya Libya.”

Waomba hifadhi wanaohamishwa kutoka Libya hupelekwa kwenye kituo cha mchakato wa dharura (ETM) kilichoko Gashora ambako kumewekwa mikakati inayozingatia hatua za kiafya za kudhibiti janga la COVID-19 ambacho kinawapa waomba hifadhi hao mazingira salama.

Waomba hifadhi hawa wataungana na kundi linguine la waomba hifadhi 184 ambao walihamishwa hapo awali ambao wanasubiri suluhu ya kudumu ya kutoka Rwanda.

Katika kituo hicho cha muda UNHCR inawapa msaada ikiwemo malazi, chakula, maji, huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na shughuli na mafunzo mbalimbali.

Wakimbizi na waomba hifadhi 44,725 wameorodheshwa na UNHCR nchini Libya na kati ya hao 329 wanashikiliwa katika mahabusu mbalimbali.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter