Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka Tigray na ujauzito hadi kujifungulia ukimbizini Sudan

Wengi wa wakimbizi wanaokimbia eneo la Tigray walioko Um Raquba ni wanawake na watoto.
© UNFPA Sudan/Sufian Abdul-Mout
Wengi wa wakimbizi wanaokimbia eneo la Tigray walioko Um Raquba ni wanawake na watoto.

Kutoka Tigray na ujauzito hadi kujifungulia ukimbizini Sudan

Wahamiaji na Wakimbizi

Kufurushwa kwa maelfu ya raia wa Ethiopia kutokana na mapigano kwenye jimbo la Tigray kumekuwa janga zaidi kwa wajawazito ambao wamejikuta wanalazimika kutembea muda mrefu na kujifungulia ugenini. Miongoni mwao ni Nigsty ambaye anasema matarajio yake ni amani irejee nyumbani ili  yeye na mwanae warejee Salama!
 

Nigsty, akiwa amebeba mwanae mchanga huyu punde baada ya kujifungulia ukimbizini nchini Sudan.
Alikimbia machafuko jimboni Tigray akatembea siku tatu..

Nigsty anasema “tuliopoondoka, nilikuwa nina njaa na uchovu. Nilikuwa pia mjamzito, kuna wakati nilianguka njiani na nyakati nilitembea bila kupumzika.”

Mama huyu ni miongoni mwa zaidi ya waethiopia 52,000 waliokimbilia Sudan na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na wadau wanawapatia msaada wa chakula, malazi, afya ,maji na huduma za kujisafi.

Hofu kubwa ni uwezekano wa mlipuko wa magonjwa miongoni mwao wanawake na watoto.

Pamoja na hofu hizo, kwa Nigsty fikra za awali zinamjia huku akishukuru.

Anasema “nilifikiria jinsi maisha yangu yalivyokuwa hatarini na kufikiria pengine nitakufa. Ulikuwa wakati mgumu sana kwangu. Ujauzito wangu ulikuwa na shida nyingi hata sikutarajia kujifungua salama.”

Mahitaij ni mengi kwa wakimbizi

Mlundikano ni mkubwa kwenye makazi haya ya wakimbizi na kuna uhaba wa dawa na vifaa vingine. Kuna mahitaji makubwa ya kuunganisha familia, elimu, nafasi rafiki kwa watoto kucheza na miradi ya lishe. Katika makazi haya ya muda ya Lugdi, wakimbizi wanaweza kupata maji safi kutoka maeneo ya jamii jirani.

Kwa Nigsty hofu yake ni mwanae ambaye anasema kitovu chake hakiko vizuri na bado hajapatiwa chanjo.

Akiwa kwenye makazi haya ya muda, Nigsty anakumbuka nyumbani..

Anasema  “mume wangu alikuwa anafanya kazi kazi kwenye shamba kama dereva wa lori. Mimi nilikuwa mama wa nyumbani. Tulikuwa na maisha mazuri. Mume wangu alileta kipato nami nilipika na kufanya usafi. Tulikuwa na maisha mazuri.”