Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa mwaka mpya 2021

Mwaka 2020 umetububujisha machozi, na kutupitisha kwenye majaribu, lakini 2021 kuna nuru- Guterres

UN News
Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa mwaka mpya 2021

Mwaka 2020 umetububujisha machozi, na kutupitisha kwenye majaribu, lakini 2021 kuna nuru- Guterres

Masuala ya UM

COVID-19 imebadili maisha yetu na kuutumbukiza ulimwengu katika mateso na huzuni. Ndivyo alivyoanza ujumbe wake wa mwaka mpya 2020, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ujumbe alioutoa kwa njia ya video kutoka jijini New York, Marekani, makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Guterres amesema, “wapendwa wengi wamepotea, na janga linaendelea kusababisha mawimbi mapya ya ugonjwa na vifo. Umasikini, pengo la usawa na njaa vinaongezeka. Ajira zinatoweka na madeni yanaongezeka. Watoto wanahaha.”

Kama hiyo haitoshi amesema, ukatili majumbani unaongezeka, na ukosefu wa usalama uko kila mahali.

Tangu kuibuka kwa COVID-19, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO linasema zaidi ya watu milioni 79 wamethibitishwa kuugua ugonjwa huo ambapo kati yao hao zaidi ya milioni 1 na nusu wamefariki dunia.

Nuru iko mbele yetu

Hata hivyo amesema “mwaka mpya uko mbele yetu. Na tunaona mwanga wa matumaini: Watu wanatoa msaada kwa majirani na wageni, wahudumu walio mstari wa mbele wanafanya kila wawezalo,  wanasayansi wanatengeneza chanjo kwa kasi iliyovunja rekodi, nchi zinatoa ahadi mpya ya kuzuia janga la mabadiliko ya tabianchi.”

Bwana Guterres amesema ikiwa watu watafanya kazi kwa umoja na mshikamano, mwangaza huo wa matumaini unaweza kufika duniani kote. Amesema hilo ndilo fundisho la mwaka huu mgumu zaidi.

Faida ya mshikamano

Katibu Mkuu amesema kwa ushirikiano na umoja, “mabadiliko ya tabianchi na janga la COVID-19 ni majanga ambayo yanaweza kushughulikiwa tu na kila mtu kwa pamoja kama sehemu ya mpito kuelekea mustakabali jumuishi na endelevu.”

Amesema ni kwa kutambua hilo, “matamanio makubwa ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2021ni kujenga  ushirikiano wa kimataifa wa kuweka mizania ya hewa ya ukaa inayozalishwa na ile inayoondolewa na hatimaye kutozalisha kabisa hewa hiyo ifikapo mwaka 2050.”

Amesema kila serikali, jiji, biashara na watu binafsi wanaweza kushiriki ili kutimiza lengo hili. “Pamoja hebu tuweke amani miongoni mwetu na mazingira, tukabili janga la mabadiliko ya tabianchi, tukomeshe kusambaa kwa COVID-19 na tuufanye mwaka 2021 kuwa mwaka wa uponjaji.”

Uponyaji kwa 2021 ni upi unaotakiwa?

Uponyaji kutokana na athari za virusi hatari, kuponya uchumi na jamii zilizosambaratika. Uponyanji wa migawanyiko na kuanza kuiponya sayari. Hilo ni lazima liwe azimio letu la mwaka mpya 2021.

Katibu Mkuu ametamatisha ujumbe wake kwa kumtakia kila mtu heri na amani kwa mwaka mpya 2021 kutoka Umoja wa Mataifa.