Skip to main content

Wakimbizi 25,000 kutoka Eritrea wapokea msaada jimboni Tigray Ethiopia:UN

Eneo la Tigray linakabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleao nchini Ethiopia. picha ya maktaba
© UNICEF/Zerihun Sewunet
Eneo la Tigray linakabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleao nchini Ethiopia. picha ya maktaba

Wakimbizi 25,000 kutoka Eritrea wapokea msaada jimboni Tigray Ethiopia:UN

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamefikisha msaada wa chakula wa kuokoa Maisha kwa wakimbizi 25,000 kutoka Eritrea walioko kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia. 

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR iliyotolewa leo mjini Addis Ababa Ethiopia msaada huo iliowasilishwa na malori 18 ambao umetolewa kwa ushirikiano na shirika la mpango wa chakula duniani WFP na shirika la Ethiopia la masuala ya wakimbizi na watu wanaorejea (ARRA) ni tani 248 za unga wa mahindi na soya, nafaka, kunde na mafuta ya kupikia na umekabidhiwa kwa mashirika ya kibinadamu ya eneo hilo kwa ajili ya kugawanywa kwa wakimbizi 13,022 wa Eritrea kwenye kambi ya Mai Ayin na tani 239 kwenye kambi ya Adi Hurush kwa ajili ya wakimbizi 12,169. 
Ann Encontre mwakilishi wa UNHCR nchini Ethiopia amesema“Familia, wanawake, wanaume, watoto na hata watoto wachanga walikuwa wamekatwa kwa msaada na huduma muhimu kwa wiki nyingi, hivyo usambazaji huu wa msaada ulikuwa unahitajika haraka”

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wakimbizi 96,000 kutoka Eritrea waliojiandikisha katika kambi nne kwenye jimbo la Tigray wanategemea msaada wa WFP ili kuweza kuishi.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa hivi sasa yanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba msaada wa kutosha wa chakula unasambazwa katika kambi zingine jimboni humo, lakini pia huduma muhimu ya ulinzi na mahitaji ya msingi kama vile malazi.

Kukiwa na mgogoro wa vita vya silaha na ripoti za mauaji ya watu wengi jimboni Tigray hofu imeongezeka kuhusu usalama wa wakimbizi.

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yamesema katika wiki saba zilizopita mapigano baina ya askari wa serikali kuu na vikosi vya jeshi la ukombozi wa watu wa Tigray (TPLF) yamewalazimisha maelfu ya watu kukimbia na kutawanywa.

Jumanne iliyopita kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet alitangaza kwamba ofisi yake imepokea madai ya ukiukwaji wa sheria za kibinadamu za kimataifa na sheria za haki za binadamu ikiwemo mashambulizi ya vifaru kwenye maeneo ya watu wengi, kuwalenga kwa makusudi raia, mauaji na kusambaa kwa vitendo vya uporaji.