Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mhudumu wa afya akisambaza vifaa vya kujisafi kwa familia moj ahuko Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh

Virusi vilivyofunga dunia: Pengo linalopanuka kati ya matajiri na maskini

UN Women/Fahad Kaizer
Mhudumu wa afya akisambaza vifaa vya kujisafi kwa familia moj ahuko Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh

Virusi vilivyofunga dunia: Pengo linalopanuka kati ya matajiri na maskini

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakati wa janga la COVID-19 pengo la ukosefu wa usawa kati ya matajiri na maskini limeongezeka zaidi, halikadhalika umaskini, ikiwa ni mara ya kwanza katika miongo kadhaa. Katika sehemu hii ya pili ya mfululizo wa makala kuhusu jinsi COVID-19 imebadili dunia, tunaangazia jinsi janga hilo limerudisha nyuma juhudi za kujenga jamii zenye usawa zaidi. 

Dunia ya mwaka 2020, ni dunia ambayo imejengwa kwenye misingi isiyo na usawa, ambapo nusu ya utajiri unamilikiwa na watu ambao wanaweza kutosha kwenye meza moja ya mkutano. Hiyo ni kauli ya António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye alitabiri kuwa takribani watu milioni 500 watakuwa bado wamesalia kwenye lindi la umaskini ifikapo mwaka 2030. 

Ukosefu wa usawa hadharani

Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, COVID-19 imeongeza pengo la ukosefu wa usawa, mtazamo ambao uliweka hadharani mwezi Februari mwaka huu  na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO, likisema kuwa watu bilioni mbili wanaofanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi ndio walioathirika zaidi.

Wachuuzi wa mboga kwenye soko moja katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
© UNICEF/NahomTesfaye
Wachuuzi wa mboga kwenye soko moja katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Mwezi Machi, shirika hilo lilirejea tena na utabiri ya kwamba mamilioni ya watu watatumbukizwa kwenye ukosefu wa ajira, au idadi ya waajiriwa itapungua au kuwa wafanyakazi maskini.

“Hili si tena janga la kiafya duniani, bali ni pia ni janga la kubwa katika soko la ajira na uchumi ambavyo vinakuwa na madhara makubwa kwa watu”, amesema Guy Rider, Mkurugenzi Mkuu wa ILO. Shirika hilo lilichapisha mapendekezo ya jinsi ya kupunguza madhara ya COVID-19 kwa mbinu za watu za kujipatia kipato, ambayo yalijumuisha kulinda ajira za wafanyakazi, vichocheo vya uchumi na ajira, pamoja na usaidizi wa kipato na ajira.

 

Mwakilishi wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP nchini Bolivia akizungumza na wanawake wa kabila la asili la Uru-Murato kuhusu uelewa wa COVID-19 na kanuni za afya na lishe.
WFP/Morelia Eróstegui
Mwakilishi wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP nchini Bolivia akizungumza na wanawake wa kabila la asili la Uru-Murato kuhusu uelewa wa COVID-19 na kanuni za afya na lishe.

Kuendeleza usambazaji wa vyakula

Ilipofika mwezi wa Aprili, kiwango cha machungu duniani kilikuwa dhahiri ambapo ripoti iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilionesha kuwa hali ya umaskini na njaa inazidi kuwa mbaya, na kwamba nchi ambazo tayari zimeathiriwa na baa la njaa zilikuwa hatarini zaidi wakati huu wa janga la Corona. “Tunapaswa kuhakikisha mnyororo wa usambazaji chakula unaendelea il iwatu waweze kupata chakula muhimu kwa uhai wao” ilisema ripoti hiyo ya utafiti ikisisitiza kuwa udharura wa kuendeleza utoaji wa misaada ya kibinadamu ili kuhakikisha watu wote waliokumbwa na janga wanapata chakula na hawafi njaa.

Kuanzia kutumia usafiri wa umma kama vituo vya mgao wa chakula, mbinu za kawaida za kusambaza vyakula majumbani, au masoko yanayofuata wateja, jamii zililazimika kusaka mbinu bunifu za kulisha walio maskini na walio hatarini, huku ikikabiliana na vikwazo vya kutembea hovyo vya COVID-19.

Hii yote ni mifano ya jinsi miji huko Amerika ya Kusini iliungana kusaidia jamii zao, na kudhihirisha maonyo ya shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, kuwa hatari za kiafya kwa wakazi wa mijini ni kubwa zaidi wakati wa COVID-19, hususan kwa watu bilioni 1.2 wanaoishi maeneo ya makazi duni au aina nyingine za makazi yasiyo rasmi.

Janga limegharimu zaidi wanawake

“Wanawake ndio wanagharimika zaidi katika janga la COVID-19 kwa kuwa wako katika nafasi kubwa zaidi ya kupoteza njia zao za kujipatia kipato na kuna nafasi finyu zaidi kwa wao kunufaika na mipango ya hifadhi ya jamii.”  Hiyo ni kauli ya Achim Steiner, Mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, akieleza madhara ya COVID-19 kwa wanawake, katika takwimu zilizotolewa mwezi Septemba.

Takwimu zilionesha kuwa viwango vya umaskini kwa wanawake viliongezeka kwa zaidi ya asilimia tisa, sawa na wanawake milioni 47: idadi inawakilisha kurejeshwa nyuma kwa mafanikio yaliyopatikana katika miongo kadhaa ya kutokomeza ufukara.

Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, amesema ongezeko la wanawake mafukara ni ukweli mchungu wa kasoro dhahiri kwenye mifumo inayounda jamii na uchumi.

Ingawa hivyo, Bwana Steiner amesisitiza kuwa mbinu zipo za kuboresha Maisha ya wanawke, hata wakati huu wa janga la sasa. Mathalani, zaidi ya wanawake na wasichana milioni 100 wanaweza kuondolewa kwenye lindi la umaskini iwapo serikali zitaimarisha fursa ya elimu na uzazi wa mpango na kuhakikisha viwango vya mshahara ni vya haki na sawa na vile vya wanaume.

Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.
WFP/Tsiory Andriantsoarana
Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.

Mtoto mmoja kati ya sita ameathirika

Maendeleo ya kupunguza umaskini miongoni mwa watoto nayo yalikwaa kisiki mwaka huu. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na Benki ya Dunia, waliripoti mwezi Oktoba ya kwamba watoto wapatao milioni 365 walikuwa wanaishi maisha ya kimaskini hata kabla ya janga la Corona, na walitabiri kwamba idadi hiyo itaongezeka kutokana na Corona.

Umaskini uliokithiri uliwanyika mamia ya mamilioni ya watoto fursa ya kufikia ustawi wao halisi, yaani kimwili na kiakili na hivyo kutishia uwezo wao wa kupata kazi nzuri utu uzimani.

“Hizi namba peke zinapaswa kumshtusha mtu yeyote”, amesema Sanjay Wijesekera, Mkurugenzi wa Miradi UNICEF: “Serikali zinapaswa kuwa na mpango wa dharura wa kunusuru na kukwamua watoto ili kuepusha watoto wengine wengi zaidi na familia zao kufikia kiwango cha umaskini ambacho hakijawahi kushuhudiwa miaka mingi.”

Misaada yavunja rekodi

Familia iliyofurushwa mjini Marib, Yemen, wakiwa wamebeba msaada waliopewa kurejea katika eneo lao la malazi
IOM
Familia iliyofurushwa mjini Marib, Yemen, wakiwa wamebeba msaada waliopewa kurejea katika eneo lao la malazi

 

Hadi mwezi Desemba, Umoja wa Mataifa ulikuwa unatabiri kuwa watu milioni 235, ambayo ni idadi kubwa kuwahi kufikiwa, watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko kwa asilimia 40 ikilinganishwa na idadi ya wale waliohitaji msaada mwaka 2020, na ongezeko hilo linachochewa na janga la Corona.
“Taswira tunayoonesha haitii kabisa moyo na ni ya giza totoro kwa mtazamo wa mahitaji ya kibinadamu kwenye  kipindi ambacho hata hatujakianza”, amesema Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya msaada wa dharura, OCHA.

Amesema hii taswira ya suala kwamba janga la COVID-19 limesababisha uharibifu mkubwa katika maeneo yote tete na yaliyo hatarini katka sayari hii ya dunia.

Bwana Lowcock ameonya kwamba kiwango cha changamoto zinazokabili watoa misaada ya kibinadamu mwakani ni kikubwa kupindukia, na kinaongezeka. “Iwapo tutavuka mwaka 2021 bila baa la njaa hayo yatakuwa mafanikio makubwa”, amesema akiongeza kuwa onyo liko dhahiri na kengele zinalia.
Wakati wa makubaliano mapya duniani

Mwishoni mwa mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alikumbusha kuwa viwango vya umaskini na ukosefu wa usawa vilivoshuhudiwa mwaka huu haviepukiki na kwamba dunia yenye usawa bado inawezena, bila kujali mishtuko mikubwa iliyotokea wakati wa janga la sasa.

Akizungumza mwezi Desemba,  Bwana Guterres ameelezea matumaini yake kuwa janga linaweza kuchochea marekebisho yanayohitajika ili kufanikisha mifumo thabiti ya hifadhi ya jamii duniain kote.

Akitafakari maoni yake ya mapema mwaka huu kuhusu ukosefu wa usawa kabla janga halijasambaa, Bwana Guterres  amesema dunia inahitaji makubaliano mapya, “ambamo kwayo madaraka, rasilimali na fursa zitagawanywa kwa usawa zaidi katika meza za maamuzi za kimataifa, na mifumo ya utawala iakisi uhalisi wa sasa”.