2020 ulikuwa mwaka wa zahma kubwa kwa wanawake na wasichana- UNFPA

24 Disemba 2020

Mwaka 2020 ukielekea ukingoni, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya idadi ya watu, UNFPA, Dkt. Natalia Kanem amesema mwaka huu wa 2020 ulikuwa ni mwaka wa janga kuu zaidi kwa wanawake na wasichana ambao tayari walikuwa kwenye masahibu hata kabla ya janga hilo.

 

Mwaka 2020, mwaka tofauti na miaka mingine kabisa!

Ndivyo anavyoanza ujumbe wake Dkt. Natalia Kanem, Mkuu wa UNFPA akitoa tathmini ya mwaka 2020 .

Anasema na janga la Corona au COVID-19, limefanya mwaka kuwa mbaya zaidi kwa wanawake na wasichana kwa kuwa anasema huduma za kuokoa maisha zilivurugwa, ukosefu wa usawa umeota kuota mizizi na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana vimeongezeka.

Ingawa hivyo anasema kwa pamoja jamii ya kimataifa iliibuka kukabili changamoto, wanawake na vijana wakisaka suluhu pale walipo na kusongesha jamii zao.

Mkurugenzi Mtendaji huyu wa UNFPA anasema shirika lake kwa upande wake mwaka huu lilifikia wanawake zaidi ya milioni 7 katika nchi 53 kwa kuwapatia huduma za afya ya uzazi .

Shirika hilo pia lilitoa huduma za uzazi wa mpango kwa watu milioni 4.4 huku watu wengine milioni 3.3 wakipatiwa huduma dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Akimulika mwaka ujao anasema, «UNFPA inaomba dola milioni 818 kulinda zaidi ya watu milioni 54, wanawake, wasichana na vijana katika nchi 68. Tunaamini katika usawa, haki na usalama kwa wote.»

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter