Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya mauaji ya raia Tigray- Bachelet

Mkimbizi wa Ethiopia kutoka jimbo la Tigray akisubiri kusafirishwa kutoka kituo cha mpakani cha mapokezi nchini Sudan.
© UNHCR/Will Swanson
Mkimbizi wa Ethiopia kutoka jimbo la Tigray akisubiri kusafirishwa kutoka kituo cha mpakani cha mapokezi nchini Sudan.

Uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya mauaji ya raia Tigray- Bachelet

Amani na Usalama

Baada ya kuibuka kwa mapigano katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia wiki saba zilizopita, kutofikishwa kwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo pamoja na kukatishwa kwa mawasiliano katika maeneo mengine vinatia wasiwasi hali ya wananchi, ameonya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa mataifa, Michelle Bachelet.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, Bi. Bachelet amenukuliwa akikaribisha tamko la serikali ya Ethiopian ikiahidi kuondoa vizuizi vyote vya kufikisha misaada ya kibinadamu, kwa kutii mkataba wa Umoja wa Mataifa uliotiiwa saini tarehe 29 Novemba mwaka huu akisema, hii inapaswa kutekelezwa katika maeneo yote ya Tigray ambako wananchi wameathiriwa na mapigano.
 
Hata hivyo amesema timu mbili za kutathimini hali ya kibinadamu zilifanikiwa kuingia Tigray hapo jana Jumatatu.
 
Bachelet amesema ofisi yake imepokea madai  kuhusu ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya ubinadamu na sheria ya haki za binadamu, ikiwemo uvurumishwaji wa mizinga ukilenga maeneo yanayohifadhi watu wengi, kuwalenga raia, mauaji ya kiholela na uporaji mkubwa wa mali.

Kamishina huyo amesema hali hii inaashiria kuwa pande zinazopigana zimeshindwa kutekeleza wajibu wao wa kulinda raia. Na kuongeza kuwa inasikitisha sana hasa wakati huu ambapo mapigano yanaripotiwa kuendelea katika maeneo ya kaskazini, katikati na kusini mwa Tigray.
 
Makumi kwa maelfu ya raia tayari wamekimbia makazi yao wakiwemo wale waliovuka mpaka na kuingia Sudan.
Bachelet pia emeeleza kuguswa kwa shirka la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), kuhusu usalama na maisha ya wakimbizi 96,000 wa Eritrea waliosajiliwa kwenye kambi nne tangu kuzuka kwa mapigano.

Wengi wa wakimbizi wanaokimbia eneo la Tigray walioko Um Raquba ni wanawake na watoto.
© UNFPA Sudan/Sufian Abdul-Mout
Wengi wa wakimbizi wanaokimbia eneo la Tigray walioko Um Raquba ni wanawake na watoto.

Ameongeza kuwa, kulingana na vizuizi vilivyopo sasa, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa haiwezi kuthibitisha habari zote zilizopo lakini imepokea mfululizo wa taarifa kuhusu ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya ubinadamu na sheria ya haki za binadamu  ukihusisha pande zote zinazopigana.
 
Mmoja wa mashahidi ameeleza mashambulio ya makombora mjini Humera kwenye mpaka wa Eritrea kati ya tarehe 9 na 11mwezi Novemba.
 
Amesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imehoji watu kadhaa amabao wamedai kuwa kombora lililovurumishwa kutoka Eritrea lilishambulia makazi na hospitali.
 
Ikiwa raia waliuawa kwa makusudi kwa kulengwa na pande moja au pande zote kwenye mzozo huo, inaweza kuwa ni uhalifu wa kivita. “ Kama nilivyosisitiza awali, uchunguzi wa kina, huru na wa wazi ufanyike ili kuwajibisha ksiheria wote waliohusika,” amesema Bachelet.