Tunachunguza aina mpya ya virusi vya Corona Uingereza na Afrika Kusini-WHO

21 Disemba 2020

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limesema linashirikiana na wanasayansi ili kuelewa aina mpya ya virusi vya COVID-19 vilivyoripotiwa huko Afrika Kusini na Uingereza.
 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa kuzingatia kuwa hivi karibuni kumekuwepo na ripoti za aina mpya za virusi SARC-CoV-2 vinavyosababisha COVID-19.

“Virusi huwa vinabadilika baada ya muda na hilo ni jambo la kawaida na lilitarajiwa” amesema Dkt. Tedros akiongeza kuwa Uingereza imeripoti aina hiyo mpya ya virusi vinavyoambukia kwa urahisi zaidi lakini hakuna ushahidi hadi sasa ya kwamba vinawaza kusababisha ugonjwa hatari zaidi au kifo.

Dkt. Tedros amesema jambo la maana ni umuhimu wa kudhibiti kuenea kwa aina zote za virusi vya SARS-CoV-2 haraka iwezekanavyo kwa kuwa kadri vinavyopata fursa ya vya kusambaa, vivyo hivyo vinakuwa na uwezo wa kubadilika.

“Siwezi kusisitiza zaidi juu ya umuhimu wa serikali na wananchi wake wote kuchukua hatua muhimu za kudhibiti kuenea kwa virusi hivi,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO.

Mwaka huu umekuwa mgumu

Mwaka huu umekuwa mgumu, tena mgumu zaidi kwa wahudumu wa afya. Msimu wa sikukuu unapoingia, zawadi pekee na bora kwa wahudumu wa afya ni kwa viongozi na wananchi wao kuchukua tahadhari na kupunguza shinikizo kwenye mifumo ya afya.

Dkt. Tedros amesema chanjo salama na fanisi “zinatupatia matumaini, lakini si kisingizio kwa watu kuachana na hatua zao za kujikinga na kujiweka kwenye hatari ya maambukizi. Sasa ni wakati wa kuongeza maradufu hatua za afya ya umma ambazo zimwezesha nchi nyingi kudhibiti virusi vya Corona.”

Fikra potofu kuwa COVID-19 inawapata wazee pekee

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amegeukia wale wanaoeneza taarifa za uongo kuwa COVID-19 inawapata wazee peke yao na kwamba kwa kuwa chanjo imepatikana basi hakuna tatizo tena. “COVID-19 inaathiri watoto na watu wazima kwa njia mbalimbali, na inaweza kushambulia mfumo wowote wa mwili. Watu wengi zaidi wanapata madhara ya muda mrefu ya Corona. Hii ni pamoja na kwenye mfumo wa fahamu kwa watoto na watu wazima, hali ambayo bado inafanyiwa utafiti.”

Chanjo ya COVID-19 na utaifa

Ingawa chanjo inatia matumaini kwa baadhi ya watu, Dkt. Tedros anasema bado ana hofu kuwa utaifa kwenye mgao na utoaji wa chanjo unaweza kuwanyima wakazi wengi maskini duniani chanjo hiyo ya kuokoa maisha.
Amesema huu ni wakati wa kubadili ahadi za kisiasa kuwa vitendo kwa kuwa ahadi pekee hazitamlinda mtu yeyote iwapo hazitimizwi.
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter