Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua mpya za usalama zaruhusu wakimbizi wa Mali kurejea kambini kutoka Burkina Faso

Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.
WFP/Mahamady Ouedraogo
Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.

Hatua mpya za usalama zaruhusu wakimbizi wa Mali kurejea kambini kutoka Burkina Faso

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limewasaidia wakimbizi 3,000 kutoka Mali kurejea kambi ya Goudoubo nchini Burkina Faso miezi tisa baada ya ukosefu wa usalama kuwalazimisha kuhama.
 

 Mwezi huu, kwa kutumia misafara ya mabasi 31 na malori, UNHCR iliwahamisha wakimbizi hao kwenda kambi ya Goudoubo iliyo kaskazini mashariki mwa nchi karibu na mji wa Dori.
 
UNHCR inasema wakimbizi wengine 150 walihama kwa hiari yao wakitumia pikipiki na teksi. Wengine walitembea kwa miguu wakiandamana na mifugo wao.
 
Goudoubo ilikuwa imewahifadhi wakimbizi 9,000 hadi mwezi Machi mwaka huu wakati mashambulizi kutoka kwa wanamgambo  yaliwalazimisha wakimbizi kuondoka.
 
Wakimbizi 5,000 walifanya uamuzi mgumu kurudi nyumbani licha ya nchi bado kukumbwa na misukosuko ambapo walisaidiwa na UNHCR.
 
Sasa mamlaka zimeongeza ulinzi ndani na maeneo yanayozunguka kambi ya Goudoubo, kukiwa na doria zaidi hatua ambayo imewawezesha wakimbizi wa mali kerejea kambini.
 
Huko Goudoubo, UNHCR na tume ya kitaifa ya wakimbizi CONAREF, wamejenga makao mpya 1,500 kwa wakimbizi wanaorudi.
 
Kando na makao, misaada muhimu, ukarabati wa miundo msingi na uboreshaji wa mitandao ya kijamii, UNHCR na wadau wamekarabati zahanati, na shule za msingi na sekondari ziko tayari kufunguliwa na kuwakaribisha tena wanafunzi.
 
Shughuli za kujipa kipato nazo zinatarajiwa kurudi zikiwemo kilimo na malisho kwa mifugo.
 
Wakimbizi wanaorudi wameanza kufungua tena biashara ndogondogo huko Goudoubo, ikiwemo maduka ya mboga na matunda na ya kuuza nyama. 

Zore Yusef wakila chakula na mmoja wa watoto wake.Mzozo wa silaha ulilazimisha familia yake kukimbia mkoa wa kaskazini wa Burkina Faso.
WFP/Marwa Awad
Zore Yusef wakila chakula na mmoja wa watoto wake.Mzozo wa silaha ulilazimisha familia yake kukimbia mkoa wa kaskazini wa Burkina Faso.


Wakimbizi wanaiambia UNHCR kuwa kurudi kambini kunamaanisha mwisho wa kuhaha kupata makazi na huduma zingine za msingi.
 
Shughuli za kuhamisha zitaendelea mwezi huu, ambao wakimbizi  2,100 zaidi wanatakiwa kureja kambi ya Goudoubo kutoka kambi ya Mentao karibu na Djibo.
 
Mawasiliano na kambi ya Mentao yamekatwa kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya mashambulizi mabaya kutatiza usambazaji wa misaada na chakula na kuwalazimu wafanyakazi wa UNHCR kusitisha shughuli zao huko.