Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za kimataifa zinahitaji suluhu ya kimataifa: Guterres aliambia Bundestag 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia bunge la Ujerumani, Bundestag.
UN WebTV
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia bunge la Ujerumani, Bundestag.

Changamoto za kimataifa zinahitaji suluhu ya kimataifa: Guterres aliambia Bundestag 

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amehutubia Bundestag ambalo ni bunge la Ujerumani ambako ameonya kuhusu mapungufu katika ushirikiano wa kimataifa na kusistiza kwamba changamoto za kimataifa zinazoikumba dunia hivi sasa zinahitaji suluhu za kimataifa. 

Miongoni mwa changamoto kubwa alizozigusia katika hotuba yake kwa bunge hilo ni pamoja na janga la Corona au COVID-19, mgogoro wa kiuchumi, kusuasua kwa mchakato wa kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs na suala la usawa wa kijinsia. 

Guterres amesema, “ni bayana kwamba njia ya kushinda mustakabali wetu ni kufunguka kwa dunia nzima. Lakini bado katika sehemu mbalimbali tunashuhudia ubinafsi wa fikra.” 

Katibu Mkuuu alialikwa kwenye bunge la Ujerumani na Rais wa bunge hilo Wolfgang Schäuble kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa . 

Chanjo kwa watu wote 

Katika hotuba yake pia mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameishukuru serikali ya Ujerumani kwa mchango na msaada wake mkubwa kwa chombo cha shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO cha kuchapuza nyenzo kwa ajili ya COVID-19 (ACT-Accelerator) na kituo chake cha COVAX kwa ajili ya kutengeneza na kugawanya kwa usawa chanjo, upimaji na matibabu ya gonjwa hilo. 

Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha kwamba kila mtu , kila mahali anaweza kupata fursa ya chanjo. 

“Changamoto yetu sasa ni kuhakikisha kwamba chanjo inachukuliwa kama ni manufaa ya umma, iweze kupatikana na kwa gharama nafuu kwa kila mtu , kila mahali. Ni chanjo ya watu wote.” 

Kupambana na virusi vya taarifa potofu 

Wakati huohuo Bwana. Guterres ameonya kwamba virusi vya utoaji taarifa potofu lazima vikomeshwe. 

“Kote duniani tumeshuhudia jinsi mitazamo mashuhuri ambayo inapuuzia sayansi inavyoupotosha umma. Imeghubikwa na taarifa za uongo na dhana potofu na mambo yamezidi kuwa mabaya.” 

Kwa mantiki hiyo Guterres ameupongeza uongozi wa Kansela Angela Merkel kwa kuchukua hatua za mapema zilizozingatia sayansi , takwimu na hatua ambazo zimechangia kupunguza maambukizi ya virusi vya COVID-19 na kuokoa Maisha ya watu wengi. 

“Utafiti unaonyesha kwamba uongozi wa wanawake wakati wa janga la COVID-19 umeleta matokeo yaliyodhahiri, endelevu na chanya.” 

Mabadiliko ya tabianchi 

Katibu Mkuu pia amezungumzia suala la usalama kutokana na mabadiliko ya tabianchi linaloambatana na mambo kama upotevu wa bayoanuai na mfumo wa maisha, ongezeko la hali ya jangwa, moto wa nyikani, mafuriko na vimbunga. 

Ametoa wito wa kuchukuliwa hatua katika maeneo matatu ambayo ni hatua za kupambana, ufadhili na kujenga mnepo wa kuhimili. 

“Ujerumani mmekuwa msitari wa mbele duniani katika kila nyanja . Tunahitaji wengine kufuata nyayo zenu na kusaidia kuunda mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya kutozalisha hewa ukaa. Nchi zote na hususan zote zenye uchumi ulioendelea lazima zijitokeze na mipango ya kufiukia lengo la kutozalisha hewa ukaa ifikapo mwaka 2050.” 

Ametoa wito wa kuchukua hatua kote duniani kuacha ufadhili wa mafuta kiskuku, kuacha kujenga motambo mipya ya kuzalisha makaa yam awe na kujumuisha mipango ya kutokomeza hewa ukaa katika program zao zote, sera na maamuzi ya maendeleo. 

Mshirika muhimu 

Guterres ameitaja Ujerumani kama mshirika muhimu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya ulinzi wa amani, ujenzi wa amani na misaada ya kibinadamu ikiwemo msaada wake katika wito wa usitishaji uhasama kimataifa uliotolewa mapema mwaka huu.