Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaonya kuhusu upungufu wa chakula kwa ajili ya wakimbizi Kenya

Mkimbizi akibeba chakula mgao uliotolewa na WFP katika kituo kambi ya Kakuma nchini Kenya.
WFP
Mkimbizi akibeba chakula mgao uliotolewa na WFP katika kituo kambi ya Kakuma nchini Kenya.

WFP yaonya kuhusu upungufu wa chakula kwa ajili ya wakimbizi Kenya

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP leo limeonya kuwa zaidi ya wakimbizi 435,000 nchini Kenya wanakabiliwa na uhaba wa chakula iwapo hautapatikana ufadhili wa dola milioni 57 kuendelea kutoa chakula Dadaab, Kakuma na Kalobeyei. 

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo mjini Nairobi Kenya, WFP imesema inahitaji dola za kimarekani milioni 57 ili kuendelea kutoa msaada wa chakula na lishe  katika ya mwezi Januari na Juni mwaka ujao wa 2021. 

Taarifa imeeleza kuwa bila ufadhili, WFP italazimika kusitisha kabisa mgao wa fedha taslimu kuanzia mwezi ujao yaani Januari na kufikia mwezi Machi, itakuwa imemaliza akiba yake yote ya chakula. Familia nyingi za wakimbizi zinategemea chakula cha WFP ili kuweza kuishi.  

Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya Lauren Landis akizungumzia maeneo makuu matatu ya wakimbizi nchini humo amesema, "WFP inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kugharamia msaada wa chakula kwa wakimbizi wanaoishi katika kambi za Dadaab na Kakuma na katika makazi ya wakimbizi ya Kalobeyei. Tumetumia rasilimali zote na kwa kweli wanakabiliwa na janga linalotishia maisha.” 

Upungufu wa fedha tayari umeilazimisha WFP kukata mgao kamili wa chakula kwa zaidi ya theluthi moja mnamo mwezi Septemba iliyopita, ikihatarisha afya na lishe ya wakimbizi. 

"Tunatoa wito kwa wafadhili wetu kutoa haraka rasilimali mpya kuturuhusu kuendelea kutoa chakula na pesa kwa wakimbizi. Usumbufu wa ukubwa huu kwa operesheni ya kuokoa maisha ya wakimbizi itakuwa janga." Landis amesema. 

Wakimbizi 40,000 wanaoishi kaskazini magharibi mwa makazi ya Kalobeyei wako hatarini kukumbana na pigo la kwanza kwani msaada wao wa chakula kutoka WFP unatolewa kwa njia yay a fedha taslimu.  

Wakimbizi wapanga foleni kupokea mgao wa chakula katika kambi ya Kakuma Kaskazini mwa Kenya.
WFP
Wakimbizi wapanga foleni kupokea mgao wa chakula katika kambi ya Kakuma Kaskazini mwa Kenya.

Katika kambi za Dadaab na Kakuma, WFP huwapatia wakimbizi karibu 400,000 msaada mchanganyiko wa pesa na chakula, lakini pesa taslimu zinachukua takribani asilimia 60 katika kapu la chakula. 

Kupunguza kwa kasi au kusimamisha kabisa msaada kunaweza kuwa na athari kubwa kwa afya na lishe ya wakimbizi na vile vile kwa hali ya utulivu na usalama katika kambi na jamii zinazozunguka. Kupunguzwa kwa mgao katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kumeongeza utapiamlo kwa watoto na akina mama. 

Pongezi kwa Kenya

WFP inaipongeza Serikali ya Kenya kwa kuendelea kuwa mwenyeji wa wakimbizi na kutafuta kutimiza majukumu yake chini muundo wa kina kuhusu namna ya kushughulikia wakimbizi, CRRF, kufungua ufikiaji wa huduma za mitaa, kutoa ardhi na kuruhusu ujumuishaji mkubwa wa wakimbizi na wakazi wa eneo hilo. 

CRRF inaelezea kujitolea kwa jumuiya ya kimataifa kukidhi mahitaji ya haraka ya kibinadamu ya wakimbizi ili kupunguza mzigo kwa Kenya. Msaada wa ziada unahitajika kuunga mkono serikali mwenyeji na nia yake njema na sio kudhoofisha mafanikio ya maendeleo.