Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nzige wa jangwani wawa tishio, kuna hofu ya kurejea tena Kenya

Mkulima katikati ya nzige wa jangwani wanaokula mazao huko kaunti ya Kitui nchini Kenya
© FAO/Sven Torfinn
Mkulima katikati ya nzige wa jangwani wanaokula mazao huko kaunti ya Kitui nchini Kenya

Nzige wa jangwani wawa tishio, kuna hofu ya kurejea tena Kenya

Tabianchi na mazingira

Wimbi la kizazi kipya cha nzige wa jangwani linatishia mbinu za kujipatia kipato wakulima na wafuaji, halikadhalika uhakika wa kupata chakula kwenye eneo la pembe ya Afrika na Yamen licha ya juhudi kubwa za shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na wadau wake.
 

FAO inasema kwa ushirikiano na wadau wa kimataifa kampeni ya aina yake iliyoratibiwa na shirika hilo imewezesha zaidi ya eka milioni 1.3 zilizokuwa zimevamiwa na nzige kwenye katika nchi 10 kudhibitiwa tangu mwezi Januari mwaka huu.

Operesheni hizo zimezuia takribani tani milioni 2.7 za nafaka kutoshambuliwa na nzige hao waharibifu, kiasi ambacho thamani yake ni takribani dola milioni 800.

FAO inasema kiasi hicho cha chakula kinatosha kulisha watu milioni 18 kwa mwaka.

Hata hivyo shirika hilo limese,a mazingira rafiki pamoja na mvua vimesababisha nzige hao kuzaliana tena mashariki mwa Ethiopia na Somalia na kwamba “hali hiyo imekuwa mbaya zaidi kutokana na kimbunga Gati ambacho kimesababisha mafuriko kaskazini mwa Somalia mwei uliopita na hivyo kupatia fursa nzige kuzaliana na idadi yao itaongezeka mwezi ujao.”

Kwa mujibu FAO kuna tishio la nzige kuvamia tena maeneo ya kaskazini mwa Kenya na pia tayari wengine wanazaliana huko Eritrea, Saudi Arabia, Sudan na Yemen.

Kwa sasa FAO inasaidia serikali na wadau wengine katika kazi ya ufuatiliaji na ushauri wa kiufundi sambamba na kupata vifaa, lakini operesheni hizo lazima ziongezewe kasi ili kuepusha kupotea kwa chakula katika nchi hizo ambazo baadhi yao tayari zinakabiliwa na uhaba wa chakula.

Tweet URL

Nchini Ethiopia, FAO inashirkiana na serikali kukabili nzige hao wa jangwani kwenye maeneo ambako tayari viwango vya ukosefu wa chakula viko juu.

Ethiopia imekuwa ikikabiliana na nzige tangu mwezi Juni mwaka jana na uwepo wa wadudu hao unatokana na mienendo ya kuvuka mipaka na mazingira rafiki kwa wadudu hao kuzaliana.

Sasa COVID-19 pamoja na uharibifu huo wa mazao umezidisha machungu kwa mamilioni ya watu.

Wananchi wapaza sauti

Foutumo Abi Dalmar, mkulima kutoka eneo la Somali nchini Ethiopia anasema maisha ya wakulima na wafugaji yamesambaratishwa, “hatuwezi kuzalisha idadi ya magunia ya shayiri ambayo tumezoea kuvuna mashambani mwetu. Mavuno hayatoshelezi si tu watoto wetu, bali pia mifugo. Sasa tuna tatizo kwenye familia, kile cha kuwapatia watoto ni kipi na kuwapatia mifugo ni kipi kwa sababu majani yaliyosalia hayatoshelezi wanyama na hakuna nafaka kwa ajili ya kulisha watoto.”

Mwakilishi wa FAO nchini Ethiopia, Fatouma Seid, amefafanua kuwa hii ni mara ya tatu eneo hilo la Somali linavamiwa na nzige, “wamekula majani ya malisho, mifugo haina chakula cha kutosha, matokeo yake familia zinazotegemea maziwa kulisha watoto wao haziwezi kupata kwa kuwa mifugo imedhoofu na haitoi maziwa. Hali hii itakuwa na madhara kwenye lishe ya watoto.”

Amesema hivi sasa wanahaha ili kuepusha tatizo la utapiamlo kwa watoto.

FAO inasema kuwa tayari imeshatumia zaidi ya dola milioni 200 kukabili nzige katika mataifa 10 ikiwemo Yemen, Ethiopia, Sudan na Somalia na kwamba mwakani 2021 wanahitaji nyongeza ya dola milioni 40 kuendeleza operesheni hiyo ya kudhibiti nzige.