Haki ya watu wa asili ya kuishi na kulisha familia zao katika mazingira yao haina mjadala:IFAD 

16 Disemba 2020

Mfuko wa kimataifa wa maendeeo ya kilimo IFAD umesema haki za watu wa jamii za asili za kuishi na kulisha familia zao kwa kutumia ardhi zao kote duniani ni suala la muhimu lisilo na mjadala na mfuko huo umezitaka serikali kote ulimwenguni kuhakikiza haki hizo zinadumishwa.

IFAD inasema kuna zaidi ya watu wa asili nusu bilioni wanaoishi katika nchi 90 duniani, na haki ya kuweza kuishi, kulima na kula lishe bora kutoka katika mazingira yao ni kitu cha muhimu na chenye thamani kubwa sana kwao. Lakini hivi sasa ardhi zao ziko katika hatari kubwa ya kupokonywa, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa kutambua hilo IFAD imeamua kuwa msitari wa mbele kufanyakazi kwa karibu na makundi ya watu wa asili  huku ikitambua kwamba watu hao ni watunzaji wa maliasili ya dunia na kukumbatia thamani ya ujuzi wao wa asili ambao ni muhimu katika kupambana na mabadiliko ya tanianchi. 

Kenya ni moja ya nchi zenye watu wa jamii za asili na Joseph Ole Simel ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la MPIDO ambalo ni la maendeleo ya wafugaji wa msitu wa Mainyoito kwenje jamii ya watu wa asili wa Kimaasai nchini humo akisistiza umuhimu wa kulinda maslahi ya jamii hizo anasema  “Kwa watu wa asili kuweza kuwa salama na kwa lishe  yao kuweza kupatikana, ulinzi wa ardhi na maliasili lazima viwe ni kipaumbele” 

Kwa mujibu wa IFAD mamilioni ya watu wa asili duniani kote wanapigania haki ya kuweza kujilisha na pia kulisha familia zao ili hatimaye wawe na uwezo wa kulinda ardhi zao, jamii zao na mfumo wao wa maisha. 

Na kuhakikisha hilo linatimizwa IFAD inafanyakazi kwa karibu na jamii hizo na hasa ikizisaidia kulinda haki zao. 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter