Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimsingi UNHCR haitakiwi iwepo iwapo tutatimiza wajibu wetu- Grandi

Wakimbizi kutoka Rwanda wakiwa wamepanga foleni nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka 1961
© UNHCR/Stanley Wright
Wakimbizi kutoka Rwanda wakiwa wamepanga foleni nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka 1961

Kimsingi UNHCR haitakiwi iwepo iwapo tutatimiza wajibu wetu- Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) limetimiza miaka 70 tangu kuanzishwa kwake ambapo Kamishna Mkuu wa shirika hilo Filippo Grandi amesema “niondoeni kwenye jukumu hili”  kwa kushughulikia visababishi vya mamilioni ya watu kukimbia makwao kutokanana vita na ukosefu wa usalama.

Katika ujumbe wake wa maadhimisho ya miaka 70 ya UNHCR , Grandi ameitaka jamii ya kimataifa ijenge dunia ambamo kwayo hakuna umuhimu wa kuwa na shirika la kuhudumia wakimbizi kwa sababu hakuna mtu yeyote atakayelazimishwa kukimbia.

“Msinielewe vibaya: kwa hali ilivyo sasa kazi yetu ni muhimu. Lakini utata ni kwamba hatupaswi kuwepo. Iwapo tutajikuta tunasherehekea zaidi siku za kuanzishwa kwa shirika hili, hitimisho ni kwamba jamii ya kimataifa imeshindwa,” amesema Grandi.

Wiki hii ni miaka 70 tangu uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa tarehe 14 Desemba 1950 wa kuanzisha ofisi ya Kamishna Mkuu wa wakimbzi, ili kusaidia mamilioni ya wakazi wa bara la Ulaya ambao walikimbia makwao kwa sababu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Awali, jukumu lake lilikuwa la muda, lakini kadri siku zilivyosonga, majukumu yameongezeka, kutokana na majanga yanayolazimu watu kukimbia makwao ili kusaka maeneo salama.

Wakimbizi takribani 200,000 wa kabila la Rohingya walimbia Myanmar miaka ya 1970 na kuingia Bangladesh
© UNHCR/L. Jenkins
Wakimbizi takribani 200,000 wa kabila la Rohingya walimbia Myanmar miaka ya 1970 na kuingia Bangladesh

Majanga mapya na magumu zaidi

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres kwa upande wake ametaja changamoto na mabadiliko ya sasa ya kazi za UNHCR.
“Hii leo mizozo inavuma mipaka na kuenea kwenye maeneo yote. Janga la tabianchi nalo linashamiri. Umaskini uliokithiri na njaa vinaongezeka, ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike unasambaa,” amesema Guterres.

Ameongeza kuwa sasa nalo ni janga la COVID-19 ambalo linaongea madhara zaidi kwa wale walio hatarini, wakiwemo wanawake, wanaume na watoto ambao wamelazimika kukimbia makwao.

Bwana Guterres ambaye yeye mwenyewe aliwahi kuwa Kamishna Mkuu wa UNHCR ametoa wito wa ushirikiano zaidi wa kimataifa ili kukabili changamoto za sasa.

 “Nasihi mataifa yarejelee upya ahadi zao kwenye mkataba wa kimataifa kwa wakimbizi; kutambua wajibu wao kwa wakimbizi na nchi zinazowahifadhi; kusaka suluhu za kudumu kwa mshikamano; haki za binadamu na utu,” amesisitiza Guterres.

Wakimbizi kutoka Ethiopia katika picha hii ya mwaka 1969 wakiwa eneo la Umm Sagatei nchini Sudan ambako walipatiwa msaada na UNHCR.
© UNHCR
Wakimbizi kutoka Ethiopia katika picha hii ya mwaka 1969 wakiwa eneo la Umm Sagatei nchini Sudan ambako walipatiwa msaada na UNHCR.

Mtu 1 kati ya 100 ni mkimbizi

Mwishoni mwa mwaka jana wa 2019, kulikuwepo na wakimbizi milioni 79.5, sawa na asilimia 1 ya wakazi wote wa dunia. Miongoni mwao takribani milioni 26 ni wakimbizi nje ya nchi zao na takribani milioni 45 ni wakimbizi wa ndani.

Halikadhalika kuna mamilioni ya watu ambao bado hawana utaifa, ambao wamenyimwa utaifia na haki za msingi za kibinadamu kama vile elimu, afya, ajira na uhuru wa kutembea.
UNHCR yenye wafanyakazi 17,300, takribani asilimia 90 wanafanya kazi zao mashinani kwenye mataifa 135.

Tweet URL

Jukumu la UNHCR si la kisiasa  

Bwana Grandi amefafanua kuwa majukumu ya UNHCR si ya kisiasa akieleza “ huwa hatupo kwenye vyumba vya mikutano wakati wa uamuzi wa mustakabali wa taifa au watu. Lakini bila shaka tupo mashinani kusaidia watu ambao wamelazimika kukimbia pindi mizozo inaposhindwa kupata suluhisho.”

Bwana Grandi amepongeza wafanyakazi waUNHCR kwa kazi zao na kwamba wajivunie vile ambavoy wanaweza kukabili changamoto.

“Iwapo pande kinzani zinakubaliana kusitisha mapigano, iwapo wakimbizi watarejea nyumbani salama, iwapo serikali zitawajibika pamoja kupatia wakimbizi hifadhi, iwapo nchi zitatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya hifadhi basi hatutakuwa na wasiwasi,” amesema Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR.