Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yalaani shambulio nchini Niger katika mji unaohifadhi wakimbizi. 

Watoto katika makazi yasiyo rasmi kwa ajili ya watu waliofurushwa na ukatili wa Boko Haram eneo la Diffa, kusini mashariki mwa Niger.
UNICEF/Vincent Tremeau
Watoto katika makazi yasiyo rasmi kwa ajili ya watu waliofurushwa na ukatili wa Boko Haram eneo la Diffa, kusini mashariki mwa Niger.

UNHCR yalaani shambulio nchini Niger katika mji unaohifadhi wakimbizi. 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Maraifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linalaani shambulio llilotekelezwa na washambuliaji wenye silaha huko Toumour, mji ulioko kusini-mashariki mwa Niger, shambulio ambalo limeua watu 28 na kujeruhi mamia wengine. 

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch amewaambia wanahabari hii leo mjini Geneva Uswisi kuwa, “UNHCR ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa wakimbizi zaidi ya 30,000 na wakimbizi wa ndani, IDPs ambao wamekuwa wakiishi Toumour.” 

Shambulio hilo lililodumu kwa saa nne, ambalo kundi la Boko Haram limedai kuhusika nalo, lilianza saa moja jioni tarehe 12 Desemba. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, washambuliaji waliharibu karibu theluthi mbili ya nyumba za mji huo, wakachoma soko la Toumour, na kuua zaidi ya ng'ombe elfu moja. Kufuatia shambulio hilo, idadi kubwa ya watu walikimbilia porini, na watu wengine wakirejeai mida ya  mchana tu. 

Toumour, kilometa 14 kutoka mpakani na Nigeria, ni mji ambao unawahifadhi wakimbizi 20,000 wa Nigeria, wakimbizi wa ndani 8,300, na wakimbizi 3,600 waliorejea ambao bado wanahitaji msaada wa kibinadamu. 

“Hadi kufikia jana Jumatatu asubuhi, Desemba 14, timu zetu na wadau wetu wameripoti kwamba watu walikuwa wakisafiri kutoka Toumour kuelekea Diffa, mji ulio umbali wa kilomita 100 na kuwakaribisha wakimbizi 46,000, wanaotafuta hifadhi, wakimbizi wa ndani, IDP, na waliorejea. Kwa pamoja na wadau wengine wa masuala ya kibinadamu na serikali za mitaa, UNHCR inaandaa makazi ya dharura, chakula, maji, na msaada wa kiafya kwa jamii zilizoathiriwa. Lakini, mafuriko makali ya hivi karibuni yamefanya iwe ngumu kwa wafanyikazi wa utoaji misaada kufika Toumour.” Ameeleza Baloch.  

UNHCR imesema eneo la Diffa kusini-mashariki mwa Niger limeathiriwa sana na kuongezeka kwa vurugu kali katika bonde la Ziwa Chad ambalo limelazimisha mamia ya maelfu kuingia katika eneo hilo. Katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, zaidi ya vitendo 450 vya mauaji, utekaji nyara, unyanyasaji wa kijinsia na kijinsia, na visa vingine vikali viliripotiwa. 

Shirika hilo la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR na wadau wake kwa sasa wanatoa ulinzi na misaada ya kibinadamu kwa zaidi ya watu 265,000 waliohamishwa kwa nguvu wakiwemo wakimbizi karibu 130,000 wa Nigeria na waomba hifadhi, watu 102,726 waliokimbia makazi yao humo humo ndani ya Niger, na waliorejea 34,324 katika eneo la Diffa. Janga la COVID-19 linazidisha ugumu wa ushughulikiaji wa tatizo kwani wengi wa wakimbizi wako makazi katika maeneo ya miji yenye watu wengi ambapo umbali kati ya mtu na mtu hauwezekani. 

“Licha ya kuongezeka kwa ukosefu wa usalama, Niger inaendelea kuonesha ukarimu kwa watu wanaokimbia vurugu katika maeneo ya Ziwa Chad na Sahel ya Niger.” UNHCR imeeleza.  

UNHCR pia inatoa wito wa kuongezwa msaada wa kifedha ili kuhakikisha mwitikio kamili kwa dharura za kibinadamu katika Bonde la Ziwa Chad, ambapo watu 300,000 wamelazimika kukimbia vurugu wakati wakimbizi na watu wengine milioni 2.9 wamefurushwa na kuwa wakimbizi wa ndani ya nchi yao. Hadi kufikia mwanzoni mwa Desemba, ni asilimia 52 tu ya dola za Kimarekani milioni 126.3 zinazohitajika kwa eneo hilo ambazo zilikuwa tayari zimetolewa.