Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walimu wanapaswa kupewa kipaumbele katika chanjo dhidi ya COVID-19:UNICEF 

Majaribio yanaonesha kwamba chanjo dhidi ya virusi vya corona ina uwezo mkubwa wa kuzuia hatariza COVID-19.
University of Oxford/John Cairns
Majaribio yanaonesha kwamba chanjo dhidi ya virusi vya corona ina uwezo mkubwa wa kuzuia hatariza COVID-19.

Walimu wanapaswa kupewa kipaumbele katika chanjo dhidi ya COVID-19:UNICEF 

Afya

Janga la corona au COVID-19 limesababisha athari kubwa katika elimu ya watoto kote duniani na kuwachanja walimu dhidi ya COVID-19 ni hatua muhimu ya kurejesha elimu ya watoto hao katika msitari unaotakiwa amesema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Bi. Henrietta Fore amesema katika kilele cha janga hilo mwishoni mwa mwezi Aprili 2020, ufungaji wa shule nchi nzima uliingilia masomo kwa karibu asilimia 90 ya wanafunzi kote duniani.  

Ameongeza kuwa wakati idadi hiyo imeanza kushuka tangu wakati huo lakini, “bado kuna dhana kwamba kufunga shule kunaweza kupunguza kusambaa kwa maambukizi licha ya kuongezeka kwa ushahidi kwamba shule sio chachu kubwa ya maambukizi katika jamii, na matokeo yake ni kwamba wakati wagonjwa wakiongezeka katika nchi nyingi duniani jamii zinaanza tena kufunga shule na tangu Desemba Mosi madarasa yamefungwa kwa karibu mtoto 1 wa shule kati ya 5 duniani kote au Watoto milioni 320.”  

Kwa mantiki hiyo mkurugenzi huyo mtendaji amesema, UNICEF inatoa wito kwa waalimu kupewa kipaumbele cha kupokea chanjo dhidi ya COVID-19 mara baada ya wahudumu wa afya walio msitari wa mbele na makundi mengine yaliyo hatarini zaidi kuchanjwa. Hii itawalinda waalimu dhidi ya virusi hivyo na kuwaruhusu kufundisha ana kwa ana na hatimaye kufungua shule.” 

Bi. Fore amesisitiza kuwa ingawa maamuzi ya mgawanjo wa chanjo hizo yako mikononi mwa serikali, “athari za kuendelea kukosa au kutohudhuria masomo ni kubwa sana hususan kwa watu wasiojiweza. Jinsi watoto wanavyoendelea kuwa nje ya shule , uwezekano wa kurejea unakuwa finyu na ndivyo inavyoendelea kuwa vigumu kwa wazazi wao kurejea kazini.” 

Ameongeza kuwa anaamini kwamba, “haya ni maamuzi magumu ambayo yanahitaji kuchukua hatua ngumu. Lakini kile ambacho hakipaswi kuwa maamuzi magumu ni kufanya kila kilicho ndani ya uwezo wetu kulinda mustakabali wa kizazi kijacho na hii inaanza kwa kuwalinda wale wanaohusika kwa kufungua mlango wa mustakabali huo wa kizazi kijacho.”