Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pengo la ujira kwa wahamiaji, linaongezeka katika nchi nyingi za kipato cha juu 

Mfanyakazi wa kiwanda cha nguo akiwa kwenye chumba anakoishi na wengine saba katika mabweni ya kiwanda cha nguo nchini Jordan.
ILO/Marcel Crozet
Mfanyakazi wa kiwanda cha nguo akiwa kwenye chumba anakoishi na wengine saba katika mabweni ya kiwanda cha nguo nchini Jordan.

Pengo la ujira kwa wahamiaji, linaongezeka katika nchi nyingi za kipato cha juu 

Wahamiaji na Wakimbizi

Ujira wa wahamiaji ugenini kwa wastani ni chini ya asilimia 13 kulinganisha na wafanyakazi wenyeji katika nchi za kipato cha juu, imesema ripoti mpya ya shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO, iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi. 

Ripoti hiyo inasema katika baadhi ya nchi pengo hilo ni kubwa, ikitolea mfano huko Cyprus ambako ni asilimia 42, Italia asilimia 30 na Austria ni asilimia 25, ingawa nchini Finland pengo la ujira kati ya mhamiaji na mwananchi ni asilimia 11 pekee. 

Ripoti imeeleza kuwa katika miaka mitano iliyopita, pengo la mishahara au ujira kwa wahamiaji limeongezeka katika nchi zenye kipato cha juu. Mathalani nchini Italia, wafanyakazi wahamiaji hupata asilimia 30 chini ya raia wa nchi hiyo, kwa mujibu wa data za hivi karibuni ikilinganishwa na asilimia 27 mnamo mwaka 2015. Nchini Ureno pengo la malipo ni asilimia 29 ikilinganishwa na asilimia 25 mwaka 2015, na nchini Ireland asilimia 21 ikilinganishwa na asilimia 19 mwaka 2015. 

Hata hivyo ripoti hiyo imesema kwa ujumla katika nchi zote wahamiaji wanakumbwa na ubaguzi na kuenguliwa na hali imekuwa mbaya zaidi hivi sasa na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19

Ripoti hiyo - Pengo la ujira kwa wahamiaji: Kuelewa tofauti za ujira kati ya wahamiaji na raia - inaonesha kwamba wahamiaji katika nchi zenye kipato cha juu wana uwezekano mkubwa wa kuwa katika kazi ya hatari, na asilimia 27 kwa mikataba ya muda na asilimia 15 wakifanya kazi kwa muda. Wako kwa idadi ndogo katika sekta za msingi kama kilimo, uvuvi na misitu na wanachukua kazi nyingi zaidi kuliko raia katika sekta kama  madini na uchimbaji mawe, utengenezaji, umeme, gesi na maji na ujenzi. 

Mkuu wa kitengo cha Ajira ya wahamiaji ILO Michelle Leighton amenukuliwa kwenye ripoti hiyo akisema, “wafanyakazi wahamiaji wanakabiliwa na ukosefu wa usawa, ikiwemo ujira wao kupuuzwa, ugumu kupata ajira na mafunzo, mazingira magumu ya kazi, ukosefu wa hifadhi ya jamii na haki za kushiriki kweye vyama vya wafanyakazi licha ya kwamba wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi wanamofanya kazi.” 

Wafanyakazi wahamiaji wanapata ujira mdogo ikilinganishwa na raia ambao wana sifa za ujuzi sawa na zao katika kazi husika. Wahamiaji wana uwezekano mkubwa wa kufanya kazi katika kazi zenye ujuzi wa chini na mshahara mdogo ambazo hazilingani na elimu na ustadi wao, hali ambayo inaweza kuashiria ubaguzi wakati wa mchakato wa kuajiriwa. Wafanyakazi wahamiaji wenye elimu ya juu katika nchi zenye kipato cha juu pia wana uwezekano mdogo wa kupata kazi katika ngazi za juu za kazi, imebainisha ripoti. 

Wafanyakazi wanawake wahamiaji wanabaguliwa mara mbili zaidi 

Wafanyakazi wanawake wahamiaji wanakabiliwa na upungufu wa ujira, maradufu, kama wahamiaji na kama wanawake. Pengo la ujira kati ya raia wa kiume na wanawake wahamiaji katika nchi zenye kipato cha juu linakadiriwa kuwa karibu asilimia 21 kwa saa. Hii ni kubwa kuliko pengo la malipo ya kijinsia, asilimia 16 katika nchi hizo. 

Mwanamke akivaa barakoa wakati akifanya kazi na kampuni yanguo ya izmir , Uturuki.
ILO/Kivanc Ozvarda
Mwanamke akivaa barakoa wakati akifanya kazi na kampuni yanguo ya izmir , Uturuki.

Athari za janga la COVID-19 

Janga la virusi vya Corona limekuwa na athari kubwa kiafya na kiuchumi kwa wafanyakazi wahamiaji kuliko kwa watu wengine wote wanaofanya kazi. Mwanzoni mwa janga la COVID-19, mamilioni ya wahamiaji walilazimika kurudi nyumbani baada ya kupoteza kazi zao. 

Kazi za wahamiaji wengi hazifanyiki kutokea majumbani ikilinganishwa na wasio wahamiaji na wengi wao hazipatikani kwa kazi ya simu ikilinganishwa na wasio wahamiaji na wengi wao ni wafanyakazi katika maeneo ambayo wanalazimika kukutana na watu hivyo kuwa hatarini kuambukizwa.  

Ripoti inahitimisha kwa kusema kuwa, janga la COVID-19, “ambalo bado hatuna picha kamili,  linaweza kupanua tofauti za soko la ajira kati ya wafanyakazi wahamiaji na raia, ambayo inaweza kuzidisha zaidi pengo la ujira.”