Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde waachilieni watoto mliowateka Nigeria:UN

Mtoto akikimbia kwenye uwanja katika kijiji jimboni Katsina, Kasakzini Magharibi mwa Nigeria.
UNICEF/Christine Nesbitt
Mtoto akikimbia kwenye uwanja katika kijiji jimboni Katsina, Kasakzini Magharibi mwa Nigeria.

Chonde chonde waachilieni watoto mliowateka Nigeria:UN

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuwaachilia mara moja na bila masharti mamia ya Watoto wavulana wanaoaminika kutekwa nyara na wanaodaiwa kuwa majambazi baada ya shambulio katika shule yao Kaskazini Magharibi mwa Nigeria. 

Imeripotiwa kwamba zaidi ya watoto 300 bado hawajulikani waliko huku wengi wakihofiwa kutekwa baada ya watu wenye silaha kuvamia shule ya wabvulana ya serikali kwenye eneo la Kankara jimbo la Katsina Ijumaa jioni saa za Nigeria.  

Kufuatia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Bwana Guterres amelaani vikali shambulio hilo na kutoa wito wa watoto hao kurejeshwa salama kwa familia zao. 

“Amerejerea kusema kwamba mashambulizi katikia shule na vituo vingine vya elimu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Ameitaka mamlaka ya Nigeria kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika na uhalifu huo.” Imeongeza taarifa yake. 

Pia Katibu Mkuu amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na msaada kwa serikali na watu wa Nigeeria katika vita vyao dhidi ya ugaidi, machafuko ya itikadi kali na uhalifu wa kupangwa. 

Ni kumbusho baya kabisa 

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limelaani shambulio hilo na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa watoto hao. 

Marie-Pierre Poire mkurugenzi wa UNICEF kwa ajili ya kanda ya Afrika Magharibi na Kati amesema kwamba shambulio hilo ni kumbusho la jinamizi kwamba utekeji wa Watoto na kusambaa kwa ukiukwaji mwingine wa haki za Watoto unaendelea kufanyika Kaskazini mwa Nigeria. 

“Watoto wanapaswa kuwa salama nyumbani, shuleni na katika maeneo ya michezo wakati wote. Tuko pamoja na familia za watoto ambao wametekwa na jamii iliyoathirika na tukio hili la kikatili.” 

Mwezi Februari mwaka 2018 wagaidi wa kundi la Boko Haram waliwateka nyara watoto wa kike waidi ya 100 kutoka shule ya sekondari ya wasichana kwenye mji wa Dapchi Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. Na miaka sita iliyopita mnamo mwaka 2014 kundi hilo la wanamgambo liliwateka wanafunzi wasichana 276 kutoka kwenye mabweni yao mjini Chibok na wengi wao hawajapatikana hadi leo.