Mradi wa kuku, mkombozi wa afya ya mama na mtoto Mvomero, Tanzania

10 Disemba 2020

Nchini Tanzania, mradi wa lishe endelevu unaoendeshwa na shirika la watoto la Save the Children kwa ufadhili wa USAID umekabidhi vifaranga vya kuku pamoja na vyakula vyake kwa serikali ya wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ili visambazwe kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya anawasili katika eneo la Wami Sokoine ambapo anapokelewa na wanajamii wengi wao ni wanawake waliobeba watoto wa umri wa kunyonya bado.  

Magari yaliyosheni maboksi yenye vifaranga vitakavyosambazwa kwa wafugaji 343 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mvomero yako hapa tayari kutimiza lengo la wananchi, wafuge, wale mayai na nyama ya kuku, na wajipatie kipato kupitia uuzaji wa bidhaa zitokanazo na kuku. 

Mkuu wa Wilaya Bwana Mgonya, kabla ya kukabidhiwa Vifaranga hivyo na Meneja wa shirika la Save the children mkoa wa Morogoro, Ndg.Nuhu Yahya, Mkuu huyo anaongea na wananchi, "msisitizo ni kwamba, vifaranga kwa maana ya kutupatia nyama ya kuku na mayai, ni sehemu ya virutubisho muhimu sana kwa maana ya chakula kwa ajili ya kutusaidia kupambana na hali ya udumavu. Hivyo napenda kutoa wito kwa wakazi wa Mvomero na jamii yote ya wakazi wa Mvomero kuhakikisha kwamba, tunatumia nyama ya kuku, na tunatumia mayai, na vyakula vingine kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaboresha hali ya lishe. Tuepukane na zile mila ambazo zinaonesha kwamba nyama ya kuku na mayai ni chakula cha kundi maalum katika jamii. Chakula hiki ni kwa ajili ya makundi yote, hususani kwa akina mama wajawazito na watoto, kuhakikisha kwamba wanawajengea uwezo hususani katika kile kipindi cha muda wa siku elfu moja, ni siku muhimu sana ambazo zinajumuisha mtoto aliyezaliwa, kuendelea kunyonya maziwa ya mama hadi miezi sita, lakini pia baada ya miezi sita, kubadilishiwa chakula mbadala, bila kusahau maziwa ya mama."

Magdalena Mapinduzi ni mmoja wa wanufaika wa mradi huu wa kuku anawashauri wengine akisema, "ninawaambia tufuge kuku, tule na nyama, tuboreshe afya, tule na mayai."

Joram Rubereje mkazi wa Wami Sokoine, ni mmoja wa wanaume wachache waliofika katika tukio hili, naye amejipatia vifaranga, anashukuru akisema, "ninashukuru sana kwanza kuwapata hawa kuku. Kuku ni moja kati ya protini au ni moja ya vyakula vinavyoweza kumwezesha mama mjamzito maisha yake yote afya yake kuwa bora. Hasa ukizingatia mtoto mdogo, kuanzia mimba hadi siku elfu  moja yaani mtoto akiwa na umri wa miaka miwili, hiki ndicho kipindi kigumu ambacho mzazi anatakiwa kuwa makini, kuweza kumfanya mtoto wako akue kiakili, kiafya na kimwili."

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter