Tamko la Haki za Binadamu ni chanjo dhidi ya madhila ya sasa- Bachelet

10 Disemba 2020

Inastaajabisha baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaendelea kupuuza ugonjwa wa Corona au COVID-19 sambamba na mbinu za rahisi za kujikinga kama kuvaa barakoa na kuepusha mikusanyiko mikubwa. Hiyo ni kauli ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet aliyotoa wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi akitoa ujumbe wake wa siku ya haki za binadamu hii leo, ujumbe ambao umemulika kwa kiasi kikubwa janga la COVID-19 na linavyosigina haki za binadamu.

Amesema “hakuna hata mmoja wetu atasahau mwaka 2020. Mwaka wa ajabu na kutisha ambao umetuachia makovu wengi wetu kwa njia mbalimbali. Takribani watu milioni 67 wameambukizwa, watu milioni 1.6 wamefariki dunia kutokana na janga hili ambalo hata dalili zake za kuondoka hazionekani.”

Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda
© UNICEF
Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda

Bi. Bachelet amesema maendeleo mengi yamerudishwa nyuma, juhudi za kutokomeza umaskini halikadhalika sambamba na hatua za kuinua hadhi ya wanawake, wasichana na watoto wa kike.

Baadhi ya wanasiasa wanabeza COVID-19

“Baadhi ya wanasiasa bado wanajadili hoja ya kujenga kinga kwa kuacha idadi kubwa ya watu waugue ugonjwa huo kana kwamba vifo vya mamia ya maelfu ya watu ni gharama ambayo inaweza kubebwa kwa maslahi ya wengi. Kuingiza siasa kwenye janga kwa njia hii ni ukosefu wa uwajibikaji na ni kosa”, amesema Bachelet.

Baya zaidi, baadhi ya viongozi wanapuuza ushahidi wa kisayansi na kuhamasisha nadharia na taarifa potofu kwa ustawi wao binafsi.

Uaminifu ‘umechomwa kisu’

Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Binadamu amesisitiza kuwa vitendo hivyo ni sawa na kutia kisu kwenye bidhaa muhimu zaidi ya uaminifu. Uaminifu kati ya mataifa na uaminifu ndani ya mataifa. Uaminifu kwa serikali, uaminifu kwa shahidi za kisayansi, uaminifu kwa chanjo, uaminifu kwa mustakabali. “Iwapo tunataka kurejesha dunia bora zaidi baada ya janga hili, kama ambavyo wazee wetu walifanya hivyo bila shaka yoyote baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, lazima tujenge tena kuaminiana baina yetu."

Bachelet na mistakabali mitatu

Bachelet amesema kwa hali ilivyo sasa  dunia inaweza kuibuka katika aina tatu za mistakabali mosi, “tunaweza kuibuka kutoka janga hili katika hali mbaya zaidi kuliko hata lilivyoanza na tukawa bado hatujajiandaa kabisa kuliko hata awali na mifumo yetu. Pili, tunaweza kuhaha sana kurejea katika hali ya kawaida, lakini hali ya kawaida ndio imetufikisha hapa tulipo sasa. Uwezekano wa tatu tunaweza kukwamuka vizuri kabisa.”
Ameongeza kuwa chanjo za kitabibu ambazo zinatengenezwa bila shaka zitakwamua dunia kutoka katika COVID-19, lakini hazitazuia au kutibu athari za kiuchumi na kijamii ambazo zimetokana na janga hili na kusababisha kuenea.

COVID-19 imeonyesha dhahiri kuenea kwa ubaguzi wa rangi
Unsplash/Thomas de Luze
COVID-19 imeonyesha dhahiri kuenea kwa ubaguzi wa rangi

Tamko la Haki za Binadamu ni chanjo tosha

Bachelet ameongeza “lakini kuna chanjo ya njaa, umaskini, ukosefu wa usawa na uwezekano, iwapo tutakuwa makini , chanjo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, halikadhalika kwa majanga mengine mengi yanayokabili utu wa kibinadamu. Ni chanjo ambayo tuliitengeneza baada ya majanga makubwa yaliyokumba dunia, ikiwemo magonjwa, majanga ya kifedha na vita kuu mbili za dunia.”

Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Binadamu ametaja chanjo hiyo kuwa ni Haki za Binadamu. Viambatano vyake vimewekwa katika Tamko la Haki za Binadamu ambalo hii leo linatimiza miaka 72 tangu kupitishwa kwake ambayo ndiyo siku ya haki za binadamu duniani.

“Tamko la haki za binadamu duniani linatekelezeka kupitia wajibu wa kila taifa ambalo limechukua hatua kuridhia mkataba mmoja au miwili ya tamko hilo ambalo linagusa maeneo yote matano ya haki za binadamu,” amesema Bi. Bachelet.

Picha ya maktaba ikionesha wakazi wa mitaa ya mabanda ya Kibera Nairobi Kenya wakipatiwa sabuni na maji kwa ajili ya kunawa mikono ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
© UNICEF
Picha ya maktaba ikionesha wakazi wa mitaa ya mabanda ya Kibera Nairobi Kenya wakipatiwa sabuni na maji kwa ajili ya kunawa mikono ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Tamko la Haki za Binadamu na mikataba mingine

Bi Bachelet amesema kuwa Tamko la Haki za Binadamu lilizaa mikataba mingine muhimu ya kimataifa kwa lengo la kulinda haki za makundi mahsusi kama vile watoto ,wanawake, watu wenye ulemavu na wahamiaji pamoja na ule unaozuia ubaguzi, umaskini na ukosefu wa maendeleo ambayo yametia mbolea na kuchochea athari za kiuchumi na kijamii zisababishwazo na COVID-19.

Amesema inastusha lakini haistaajabishi kuona kuwa janga la Corona limekuwa na athari tofauti tofauti kimakundi, likigusa zaidi watu ambao tayari wa pembezoni na ambao wanakabiliwa tayari na ubaguzi hususan watu wenye asili ya Afrika, makabila madogo na watu wa asili.

“Hii imekuwa dhahiri katika baadhi ya nchi tajiri zaidi, ambako kiwango cha vifo kwa baadhi ya makundi ya watu wa rangi fulani au kabila dogo imekuwa mara tatu zaidi ya jamii nzima,”amefafanua Bi. Bachelet.

Makundi hayo yamekumbwa na maambukizi zaidi kutokana na kazi zao wanazofanya ambazo pia ni za ujira mdogo ingawa hivi sasa kazi zao hizo zinatambuliwa kuwa ni muhimu; wahudumu wa afya, wasafishaji, wasafirishaji, wauzaji kwenye maduka ambao wengi wao wanatoka katika makundi hayo madogo.
COVID-19 yafanya maskini kuwa maskini zaidi

Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu amesema “kwa kipindi cha zaidi ya miezi 11, maskini wamezidi kuwa maskini na wale wanaokabiliwa na ubaguzi wamezidi kukumbwa na ubaguzi.”

Akimulika mwelekeo wa mbele, Bi. Bachelet amesema nchi tajiri lazima zisaidie nchi maskini ili kujikwamua vyema kutoka katika janga la sasa sambamba na kurekebisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa ambao sasa umekumbwa na majeraha.

Chanjo dhidi ya virusi vya Corona iliyotengenezwa na chuo cha Oxford.
University of Oxford/John Cairns
Chanjo dhidi ya virusi vya Corona iliyotengenezwa na chuo cha Oxford.

Tuchukue hatua sasa au tutumbukie kwenye kiama

Bi. Bachelet amehoji, “Je tunaweza kutumia furs aya sasa kubadilisha mwelekeo na kukwamuka vyema zaidi? Je tunaweza kutumia vyema chanjo yetu ya haki za binadamu ambayo itatusaidia kujenga jamii yenye mnepo zaidi na ya ustawi na jumuishi? Je tunaweza kuchukua hatua za haraka na muhimu kukabili kitisho kikubwa zaidi hivi sasa cha mabadiliko ya tabianchi? Hebu na tuwe na matumaini hayo. Kwa sababu iwapo hatuna hususan kwa kuangalia mabadiliko ya tabianchi, mwaka 2020 bila shaka utakuwa ndio hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye kiama!”
Tamko la Haki za Binadamu ndio nyaraka inayoripotiwa kuwa imetafsiriwa kwa lugha nyingi zaidi duniani ikiwemo kiswahili.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter