Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huwezi kusema jamii yako imeendelea kama hujatimiza SDGs-They Need Us Initiative 

Vijana waanzilishi wa asasi ya “They Need Us Initiative” yenye lengo la kuhamasisha vijana kushiriki katika jamii zao kuifanya dunia kuwa mahali bora pa kuishi.
UN Tanzania
Vijana waanzilishi wa asasi ya “They Need Us Initiative” yenye lengo la kuhamasisha vijana kushiriki katika jamii zao kuifanya dunia kuwa mahali bora pa kuishi.

Huwezi kusema jamii yako imeendelea kama hujatimiza SDGs-They Need Us Initiative 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania, vijana waanzilishi wa asasi ya “They Need Us Initiative” yenye lengo la kuhamasisha vijana kushiriki katika jamii zao kuifanya dunia kuwa mahali bora pa kuishi, wametoa wito kwa wadau mbalimbali kuwaunga mkono katika mkutano wao utakaofanyika mwishoni mwa wiki ijayo. 

Charles Michael ambaye ni Mwenyekiti wa asasi hiyo anaeleza kuwa suala la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, litapewa kipaumbele katika mkutano wao huo, “hakuna shaka kuwamba Malengo ya maendeleo endelevu yana mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi wan chi yoyote duniani, kwa ustawi wa jamii ya vijana wan chi yoyote duniani. Hauwezi ukasema una nchi ya watu wanaojenga uchumi endapo nchi yako ina janga la njaa. Huwezi ukasema una vijana ambao wanatengeneza nguvu kazi ya taifa endapo nchi yako haina amani. Huwezi ukasema nchi yako imeendelea lakini ina masuala ya unyanyasaji wa kijinsia. Na haya yote yameangaziwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu. Hii yote tutaenda kugusia katika huo mkutano. Kwamba kuna namna gani kati ya Malengo endelevu na uchumi w anchi na wao vijana kwenda kwenye jamii yao.” 

Afisa Programu wa asasi hiyo Christina Godfrey anasema sasa wameamua kukutana ana kwa ana ingawa tayari walikuwa wameanza kuelimishana kupitia teknolojia ya simu,“kabla ya mkutano huu unaokuja, tulikuwa tunafanya madarasa ya mtandaoni, kwamba tunatafuta mada tunafundishana kwa njia ya WhatsApp, kuna ukatili wa kiafya, kuna ukatili wa kimwili, kuna ukatili wa kiuchumi, kingono pia kimwili. Kwa hivyo sisi kama ‘They Need Us’, tumeweza kutoa elimu zaidi kwamba wanawake, wanaume au vijana kwa ujumla wasibweteke majumbani, waweze kutetea haki zao na pia kuwaonesha ni wapi waende pale wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia.”